Rukia maudhui

Mithali23

Busara Unapokula na Watawala

1
Uketipo kula chakula na mtawala, angalia vyema kile kilicho mbele yako,
2
na utie kisu kooni mwako kama ukiwa mlafi.
3
Usitamani vyakula vyake vitamu kwa kuwa chakula hicho ni cha hila.

Upumbavu wa Kukimbilia Utajiri

4
Usijitaabishe ili kuupata utajiri, uwe na hekima kuonyesha kujizuia.
5
Kufumba na kufumbua utajiri hutoweka, huwa kama umepata mabawa ghafula, ukaruka na kutoweka angani kama tai.

Jiepushe na Mwenye Karoho na Hila

6
Usile chakula cha mtu mchoyo, usitamani vyakula vyake vitamu,
7
kwa maana yeye ni aina ya mtu ambaye kila mara anafikiri juu ya gharama. Anakuambia, “Kula na kunywa,” lakini moyo wake hauko pamoja nawe.
8
Utatapika kile kidogo ulichokula, nawe utakuwa umepoteza bure maneno yako ya kumsifu.

Hekima kwa Wasikilizaji Tofauti

9
Usizungumze na mpumbavu, kwa maana atadhihaki hekima ya maneno yako.

Heshimu Mipaka na Maskini

10
Usisogeze jiwe la mpaka wa zamani wala kunyemelea kwenye mashamba ya yatima,
11
kwa kuwa Mtetezi wao ni mwenye nguvu, atalichukua shauri lao dhidi yako.

Kujitoa kwa Mafundisho

12
Elekeza moyo wako kwenye mafundisho na masikio yako kwenye maneno ya maarifa.
13
Usimnyime mtoto adhabu, ukimwadhibu kwa fimbo, hatakufa.
14
Mwadhibu kwa fimbo na kuiokoa nafsi yake kutoka mautini.
15
Mwanangu, kama moyo wako una hekima, basi moyo wangu utafurahi,
16
utu wangu wa ndani utafurahi, wakati midomo yako itakapozungumza lililo sawa.

Usiwahusudu Wenye Dhambi

17
Usiuruhusu moyo wako kuwaonea wivu wenye dhambi, bali kila mara uwe na bidii katika kumcha Bwana.
18
Hakika kuna tumaini la baadaye kwa ajili yako, nalo tarajio lako halitakatiliwa mbali.

Jiepushe na Ulevi na Ulafi

19
Sikiliza, mwanangu na uwe na hekima, weka moyo wako kwenye njia iliyo sawa.
20
Usiwe miongoni mwa wanywao mvinyo, au wale walao nyama kwa pupa,
21
kwa maana walevi na walafi huwa maskini, nako kusinzia huwavika matambara.
22
Msikilize baba yako, aliyekuzaa, wala usimdharau mama yako atakapokuwa mzee.
23
Nunua kweli wala usiiuze, pata hekima, adabu na ufahamu.
24
Baba wa mwenye haki ana furaha kubwa, naye aliye na mwana mwenye hekima humfurahia.
25
Baba yako na mama yako na wafurahi, mama aliyekuzaa na ashangilie!

Hatari ya Uasherati

26
Mwanangu, nipe moyo wako, macho yako na yafuate njia zangu,
27
kwa maana kahaba ni shimo refu na mwanamke mpotovu ni kisima chembamba.
28
Kama mnyangʼanyi, hungojea akivizia, naye huzidisha wasio waaminifu miongoni mwa wanaume.

Orodha ya Taabu za Ulevi

29
Ni nani mwenye ole? Ni nani mwenye huzuni? Ni nani mwenye ugomvi? Ni nani mwenye malalamiko? Ni nani aliye na majeraha yasiyo na sababu? Ni nani mwenye macho mekundu?
30
Ni hao wakaao sana kwenye mvinyo, hao waendao kuonja mabakuli ya mvinyo uliochanganywa.
31
Usiukodolee macho mvinyo wakati ukiwa mwekundu, wakati unapometameta kwenye bilauri, wakati ushukapo taratibu!
32
Mwishowe huuma kama nyoka na kutia sumu yake kama nyoka mwenye sumu.
33
Macho yako yataona mambo mageni na moyo wako kuwazia mambo yaliyopotoka.
34
Utakuwa kama alalaye katikati ya bahari, alalaye juu ya kamba ya merikebu.
35
Utasema, “Wamenipiga lakini sikuumia! Wamenichapa, lakini sisikii! Nitaamka lini ili nikanywe tena?”
Use arrow keys to navigate
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Reading Width 45 chars

Options