Rukia maudhui

circa 1380–1050 BC

The Judges & Ruth

Israel cycles through rebellion, oppression, and rescue under charismatic leaders—culminating in Ruth's faithful love story.

703 mistari · 2 vitabu vimehusishwa

Mistari ya kipindi hiki

Chuja kwa kitabu
  1. Waamuzi 14:1takriban 1141 KK

    Samsoni akateremkia Timna, akamwona mwanamke wa Kifilisti.

  2. Waamuzi 14:2takriban 1141 KK

    Alipopanda kutoka huko, akawaambia baba yake na mama yake, “Nimemwona mwanamke wa Kifilisti huko Timna; basi mnipe ili awe mke wangu.”

  3. Waamuzi 14:3takriban 1141 KK

    Baba yake na mama yake wakamjibu, “Je, hakuna mwanamke miongoni mwa jamaa yako au miongoni mwa ndugu zako, hata ulazimike kwenda kujitwalia mwanamke kutoka kwa hawa Wafilisti wasiotahiriwa?” Lakini Samsoni akamwambia baba yake, “Nipatieni huyo kwa maana ndiye alinipendeza.”

  4. Waamuzi 14:4takriban 1141 KK

    (Baba yake na mama yake hawakujua kuwa jambo hili limetoka kwa Bwana, kwani alikuwa akitafuta sababu ya kukabiliana na Wafilisti; kwa kuwa wakati huo walikuwa wakiwatawala Waisraeli.)

  5. Waamuzi 14:5takriban 1141 KK

    Samsoni akateremkia Timna pamoja na baba yake na mama yake. Walipofika kwenye mashamba ya mizabibu huko Timna, ghafula mwana simba akamjia akimngurumia.

  6. Waamuzi 14:6takriban 1141 KK

    Roho wa Bwana akaja juu yake kwa nguvu, naye akampasua yule simba kwa mikono yake bila silaha yoyote kama vile mtu ampasuavyo mwana-mbuzi, wala hakumwambia baba yake wala mama yake aliyoyafanya.

  7. Waamuzi 14:7takriban 1141 KK

    Basi akateremka na kuongea na yule mwanamke, naye akampendeza Samsoni.

  8. Waamuzi 14:8takriban 1141 KK

    Baada ya muda aliporudi ili akamwoe, akatazama kando ili kuutazama mzoga wa yule simba, na tazama, kulikuwa na kundi la nyuki ndani ya ule mzoga wa simba na kulikuwa na asali;

  9. Waamuzi 14:9takriban 1141 KK

    akachukua asali mkononi mwake akaendelea huku akila. Alipowafikia baba yake na mama yake, akawapa ile asali nao wakala. Lakini hakuwaambia kuwa alitwaa asali kutoka kwenye mzoga wa simba.

  10. Waamuzi 14:10takriban 1141 KK

    Basi baba yake akateremka kumwona huyo mwanamke. Samsoni akafanya karamu huko, kama ilivyokuwa desturi ya vijana.

  11. Waamuzi 14:11takriban 1141 KK

    Watu walipomwona, wakaleta vijana wenzake thelathini ili kuwa pamoja naye.

  12. Waamuzi 14:12takriban 1141 KK

    Samsoni akawaambia, “Niwape kitendawili, mkiweza kunipa jibu katika muda wa siku hizi saba za karamu, nitawapa mavazi thelathini ya kitani na mavazi mengine mivao thelathini.

  13. Waamuzi 14:13takriban 1141 KK

    Lakini msipoweza kufumbua, ndipo ninyi mtanipa mavazi thelathini ya kitani na mavazi mengine mivao thelathini.” Wakamwambia, “Tuambie hicho kitendawili, hebu na tukisikie.”

  14. Waamuzi 14:14takriban 1141 KK

    Akawaambia, “Ndani ya mlaji, kulitoka kitu cha kuliwa, ndani ya mwenye nguvu, kulitoka kitu kitamu.” Kwa muda wa siku tatu hawakuweza kutoa jibu.

  15. Waamuzi 14:15takriban 1141 KK

    Siku ya saba, wakamwambia mkewe Samsoni, “Mbembeleze mumeo ili atueleze hicho kitendawili, la sivyo tutakuchoma moto wewe na wa nyumba ya baba yako. Je, mmetualika ili mpate kutunyangʼanya kile tulicho nacho?”

  16. Waamuzi 14:16takriban 1141 KK

    Basi mke wa Samsoni akalia mbele yake na kumwambia, “Unanichukia! Hunipendi kabisa. Umewategea watu wangu kitendawili, lakini mimi hujaniambia jibu.” Samsoni akamwambia, “Wala sijamweleza baba yangu wala mama yangu, kwa nini nikufumbulie?”

  17. Waamuzi 14:17takriban 1141 KK

    Mkewe akalia kwa muda wa zile siku zote saba za karamu. Hivyo siku ile ya saba Samsoni akamweleza, kwa kuwa aliendelea kumsisitiza sana. Naye akawaeleza watu wake kile kitendawili.

  18. Waamuzi 14:18takriban 1141 KK

    Siku ya saba kabla ya jua kutua, watu wa mji wakamwambia Samsoni, “Ni nini kitamu kama asali? Ni nini chenye nguvu kama simba?” Samsoni akawaambia, “Kama hamkulima na mtamba wangu, hamngeweza kufumbua kitendawili changu.”

  19. Waamuzi 14:19takriban 1141 KK

    Ndipo Roho wa Bwana akamjia Samsoni kwa nguvu. Akateremka mpaka Ashkeloni, akawaua watu waume thelathini miongoni mwa watu wa mji, akatwaa mali zao na nguo zao, akawapa watu wale waliofumbua kile kitendawili. Akiwa na hasira, akakwea kurudi nyumbani kwa baba yake.

  20. Waamuzi 14:20takriban 1141 KK

    Lakini huyo mke wa Samsoni akakabidhiwa kwa rafiki yake Samsoni ambaye alikuwa rafiki yake msaidizi siku ya arusi.

  21. Waamuzi 15:1takriban 1141 KK

    Baada ya kitambo kidogo, wakati wa mavuno ya ngano, Samsoni akachukua mwana-mbuzi, kwenda kumzuru mkewe. Akasema, “Nataka kuingia chumbani kwa mke wangu.” Lakini baba yake huyo mwanamke hakumruhusu kuingia.

  22. Waamuzi 15:2takriban 1141 KK

    Huyo baba mkwe wake akamwambia, “Nilikuwa na hakika kwamba ulimkataa, hivyo mimi nikampa rafiki yako. Je, mdogo wake wa kike si mzuri zaidi kuliko yeye? Mchukue huyo badala yake.”

  23. Waamuzi 15:3takriban 1141 KK

    Samsoni akawaambia, “Wakati huu, nitakapowadhuru Wafilisti, sitakuwa na lawama.”

  24. Waamuzi 15:4takriban 1141 KK

    Hivyo Samsoni akatoka akawakamata mbweha 300 na kuwafunga wawili wawili kwa mikia yao kila mmoja kwa mwingine. Kisha akafungia mwenge wa moto, kwenye mikia ya kila jozi moja ya mbweha aliyokuwa ameifunga,

  25. Waamuzi 15:5takriban 1141 KK

    akawasha ile mienge na kuwaachia wale mbweha katika mashamba ya Wafilisti ya nafaka zilizosimamishwa katika matita. Akateketeza matita ya nafaka zilizosimama, pamoja na mashamba ya mizabibu na viunga vya mizeituni.