Skip to content

Mistari ya Biblia kuhusu The Second Temple

134 mistari · 49 vipengele

Mistari muhimu ya Biblia

Chuja kwa kitabu
  1. Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi, ili kulitimiza neno la Bwana lililosemwa na nabii Yeremia, Bwana aliusukuma moyo wa Koreshi mfalme wa Uajemi kutangaza katika himaya yake yote kwa maandishi:

  2. “Hili ndilo asemalo Koreshi mfalme wa Uajemi: “ ‘Bwana, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote duniani, na ameniagiza kumjengea Hekalu huko Yerusalemu katika Yuda.

  3. Yeyote wa watu wake miongoni mwenu, Mungu wake na awe pamoja naye, wacha apande kwenda Yerusalemu katika Yuda na kujenga Hekalu la Bwana, Mungu wa Israeli, Mungu aliyeko huko Yerusalemu.

  4. Nao watu wa mahali popote wale walionusurika wanapoishi sasa, watu hao wampe fedha na dhahabu, pamoja na vifaa na mifugo, mbali na sadaka za hiari kwa ajili ya Hekalu la Mungu huko Yerusalemu.’ ”

  5. Zaidi ya hayo, Mfalme Koreshi akavitoa vyombo vilivyokuwa mali ya Hekalu la Bwana, ambavyo Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka Yerusalemu na kuviweka katika hekalu la mungu wake.

  6. Koreshi mfalme wa Uajemi akavitoa kwa mkono wa Mithredathi mtunza hazina, aliyevihesabu mbele ya Sheshbaza mkuu wa Yuda.

  7. Hii ilikuwa ndio orodha ya vifaa: masinia ya dhahabu yalikuwa 30 masinia ya fedha yalikuwa 1,000 vyetezo vya fedha vilikuwa 29

  8. mabakuli ya dhahabu yalikuwa 30 mabakuli ya fedha yanayofanana yalikuwa 410 vifaa vingine vilikuwa 1,000.

  9. Kwa ujumla, kulikuwa na vyombo 5,400 vya dhahabu na vya fedha. Sheshbaza akavileta hivi vyote wakati watu walipotoka uhamishoni Babeli kwenda Yerusalemu.

  10. Mwezi wa saba ulipowadia baada ya Waisraeli kukaa katika miji yao, watu wote walikusanyika huko Yerusalemu kama mtu mmoja.

  11. Yeshua mwana wa Yosadaki na makuhani wenzake, Zerubabeli mwana wa Shealtieli pamoja na wenzake walianza kujenga madhabahu ya Mungu wa Israeli ili kumtolea dhabihu za sadaka za kuteketezwa kwa moto juu yake, kulingana na ilivyoandikwa katika Sheria ya Mose mtu wa Mungu.

  12. Ingawa waliwaogopa watu waliowazunguka, walijenga madhabahu juu ya ule msingi wake, wakamtolea Bwana dhabihu za sadaka za kuteketezwa kwa moto juu yake za asubuhi na za jioni.

  13. Kisha kulingana na kile kilichoandikwa, wakaiadhimisha Sikukuu ya Vibanda wakitoa idadi ya sadaka za kuteketezwa kama ilivyohitajika kila siku sawasawa na ilivyoagizwa.

  14. Baada ya hayo, walitoa sadaka za kuteketezwa za kawaida, sadaka za Mwezi Mwandamo na dhabihu zote za sikukuu takatifu za Bwana zilizoamriwa, pamoja na zile sadaka za hiari zilizotolewa kwa Bwana.

  15. Ingawa bado msingi wa Hekalu la Bwana ulikuwa haujawekwa, watu walianza kutoa sadaka za kuteketezwa kwa moto kwa Bwana tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba.

  16. Kisha watu wakawapa mafundi wa uashi na useremala fedha, wakawapa watu wa Sidoni na Tiro vyakula, vinywaji na mafuta ili waweze kuleta magogo ya mierezi kwa njia ya bahari kutoka Lebanoni hadi Yafa, kama alivyoagiza Koreshi mfalme wa Uajemi.

  17. Katika mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya Waisraeli kufika kwenye nyumba ya Mungu huko Yerusalemu, Zerubabeli mwana wa Shealtieli, Yeshua mwana wa Yosadaki na ndugu zao wengine (makuhani, Walawi na wote waliorejea Yerusalemu kutoka uhamishoni) walianza kazi, wakiteua Walawi wenye umri kuanzia miaka ishirini au zaidi kusimamia ujenzi wa nyumba ya Bwana.

  18. Yeshua na wanawe, pamoja na ndugu zake, Kadmieli na wanawe (wazao wa Hodavia), wana wa Henadadi na wana wao na ndugu zao, Walawi wote walijiunga pamoja kusimamia wale waliofanya kazi katika nyumba ya Mungu.

  19. Wajenzi walipoweka msingi wa Hekalu la Bwana, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao wakiwa na tarumbeta na Walawi (wana wa Asafu) wakiwa na matoazi, walishika nafasi zao za kumtukuza Bwana, kama ilivyoagizwa na Daudi mfalme wa Israeli.

  20. Waliimba nyimbo za sifa na za shukrani kwa Bwana hivi: “Yeye ni mwema; upendo wake kwa Israeli wadumu milele.” Watu wote wakapaza sauti kubwa za sifa kwa Bwana, kwa sababu msingi wa nyumba ya Bwana ulikuwa umewekwa.

  21. Lakini wengi wa makuhani wazee, Walawi na viongozi wa jamaa waliokuwa wameona Hekalu la mwanzoni, walilia kwa sauti walipoona msingi wa Hekalu hili ukiwekwa, huku wengine wengi wakipiga kelele kwa furaha.

  22. Hakuna mtu ambaye angeweza kutofautisha sauti hizo za furaha na za kilio, kwa sababu watu walipiga kelele sana. Nayo hiyo sauti ikasikika mbali.

  23. Adui za Yuda na Benyamini waliposikia kwamba watu waliorudi kutoka uhamishoni wanajenga Hekalu kwa ajili ya Bwana, Mungu wa Israeli,

  24. wakamjia Zerubabeli na viongozi wa jamaa, nao wakasema, “Turuhusuni tuwasaidie kujenga, kwa sababu sisi tunamtafuta Mungu wenu kama ninyi na tumekuwa tukimtolea dhabihu tangu wakati wa Esar-Hadoni mfalme wa Ashuru, aliyetuleta hapa.”

  25. Lakini Zerubabeli, Yeshua na viongozi wengine wa jamaa ya Israeli wakawajibu, “Ninyi hamna sehemu nasi katika kujenga Hekalu la Mungu wetu. Sisi peke yetu tutajenga Hekalu kwa ajili ya Bwana, Mungu wa Israeli, kama Mfalme Koreshi, mfalme wa Uajemi alivyotuagiza.”