God
Mistari inayomtaja God
Nitangʼoa nguzo za Ashera katikati yenu na kubomoa miji yenu.
Nitalipiza kisasi kwa hasira na ghadhabu juu ya mataifa ambayo hayajanitii.”
Sikiliza asemalo Bwana: “Simama, tetea shauri lako mbele ya milima; vilima na visikie lile unalotaka kusema.
Sikilizeni, ee milima, mashtaka ya Bwana, sikilizeni, enyi misingi ya milele ya dunia. Kwa kuwa Bwana ana shauri dhidi ya watu wake; anatoa mashtaka dhidi ya Israeli.
“Watu wangu, nimewatendea nini? Nimewalemea kwa jinsi gani? Mnijibu.
Nimewatoa kutoka Misri na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa. Nilimtuma Mose awaongoze, pia Aroni na Miriamu.
Watu wangu, kumbukeni jinsi Balaki mfalme wa Moabu alivyofanya shauri na kile Balaamu mwana wa Beori alichojibu. Kumbukeni safari yenu kutoka Shitimu mpaka Gilgali, ili mfahamu matendo ya haki ya Bwana.”
Nimjie Bwana na kitu gani na kusujudu mbele za Mungu aliyetukuka? Je, nije mbele zake na sadaka za kuteketezwa, nije na ndama za mwaka mmoja?
Je, Bwana atafurahishwa na kondoo dume elfu, au mito elfu kumi ya mafuta? Je, nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa ajili ya kosa langu, mtoto wangu mwenyewe kwa ajili ya dhambi ya nafsi yangu?
Amekuonyesha yaliyo mema, ee mwanadamu. Bwana anataka nini kwako? Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.
Sikiliza! Bwana anauita mji: kulicha jina lako ni hekima: “Tii hiyo fimbo na yeye aliyeiamuru.
Je, naweza kuhukumu kuwa mtu mwenye mizani ya udanganyifu hana hatia, aliye na mfuko wa mawe ya kupimia ya uongo?
Kwa hiyo, nimeanza kukuharibu, kuwaangamiza kwa sababu ya dhambi zenu.
Mtakula lakini hamtashiba; matumbo yenu bado yatakuwa matupu. Mtaweka akiba lakini hamtaokoa chochote, kwa sababu mtakachoweka akiba nitatoa kwa upanga.
Mmezishika sheria za Omri na matendo yote ya nyumba ya Ahabu, tena umefuata desturi zao. Kwa hiyo nitakutoa kwa maangamizi na watu wako kuwa dhihaka; mtachukua dharau za mataifa.”
Lakini mimi, namtazama Bwana kwa matumaini, namngoja Mungu Mwokozi wangu; Mungu wangu atanisikia mimi.
Usifurahie msiba wangu, ee adui yangu! Ingawa nimeanguka, nitainuka. Japo ninaketi gizani, Bwana atakuwa nuru yangu.
Kwa sababu nimetenda dhambi dhidi yake, nitabeba ghadhabu ya Bwana, mpaka atakaponitetea shauri langu na kuithibitisha haki yangu. Atanileta nje kwenye mwanga, nami nitaiona haki yake.
Kisha adui yangu ataliona naye atafunikwa na aibu, yule aliyeniambia, “Yu wapi Bwana Mungu wako?” Macho yangu yataona kuanguka kwake, hata sasa atakanyagwa chini ya mguu kama tope barabarani.
Wachunge watu wako kwa fimbo yako, kundi la urithi wako, ambalo linaishi peke yake msituni, katika nchi ya malisho yenye rutuba. Waache walishe katika Bashani na Gileadi kama ilivyokuwa siku za kale.
“Kama siku zile mlipotoka Misri, nitawaonyesha maajabu yangu.”
Wataramba mavumbi kama nyoka, kama viumbe vitambaavyo juu ya ardhi. Watatoka nje ya mapango yao wakitetemeka; watamgeukia Bwana Mungu wetu kwa hofu nao watakuogopa.
Ni nani Mungu kama wewe, ambaye anaachilia dhambi na kusamehe makosa ya mabaki ya urithi wake? Wewe huwi na hasira milele, bali unafurahia kuonyesha rehema.
Utatuhurumia tena, utazikanyaga dhambi zetu chini ya nyayo zako, na kutupa maovu yetu yote katika vilindi vya bahari.
Utakuwa wa kweli kwa Yakobo, nawe utamwonyesha Abrahamu rehema, kama ulivyowaahidi kwa kiapo baba zetu siku za kale.