Hesabu 32:16-32
16
Ndipo wakamjia Mose na kumwambia, “Tungalitaka kujenga mazizi hapa kwa ajili ya mifugo yetu na miji kwa ajili ya wanawake wetu na watoto.
17
Lakini sisi tuko tayari kuchukua silaha zetu na kutangulia mbele ya Waisraeli mpaka tutakapowaleta mahali pao. Wakati huo wanawake wetu na watoto wataishi katika miji yenye ngome, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya wenyeji wa nchi.
18
Hatutarudi nyumbani mwetu mpaka kila Mwisraeli apokee urithi wake.
19
Hatutapokea urithi wowote pamoja nao ngʼambo ya Yordani, kwa sababu urithi wetu umekuja kwetu upande wa mashariki ya Yordani.”
20
Kisha Mose akawaambia, “Kama mtafanya jambo hili, kama mtajivika silaha mbele za Bwana kwa ajili ya vita,
21
na kama ninyi nyote mtakwenda mmejivika silaha ngʼambo ya Yordani mbele za Bwana mpaka awe amewafukuza adui zake mbele zake,
22
hadi wakati nchi itakapokuwa imeshindwa mbele za Bwana, ndipo mtaweza kurudi na kuwa huru kutoka masharti yenu kwa Bwana na Israeli. Nayo nchi hii itakuwa milki yenu mbele za Bwana.
23
“Lakini mkishindwa kufanya hili, mtakuwa mnatenda dhambi dhidi ya Bwana; nanyi kuweni na hakika kuwa dhambi yenu itawapata.
24
Jengeni miji kwa ajili ya wanawake na watoto wenu, na mazizi kwa ajili ya mbuzi na kondoo zenu, lakini fanyeni yale mliyoahidi.”
25
Wagadi na Wareubeni wakamwambia Mose, “Sisi watumishi wako tutafanya kama bwana wetu anavyotuagiza.
26
Watoto na wake zetu, makundi ya mbuzi na kondoo, na makundi ya ngʼombe zetu, watabaki hapa katika miji ya Gileadi.
27
Lakini watumishi wenu, kila mwanaume aliyevaa silaha za vita, watavuka ngʼambo kupigana mbele za Bwana, sawa kama bwana wetu anavyosema.”
28
Kisha Mose akatoa amri kuhusu wao kwa kuhani Eleazari, na Yoshua mwana wa Nuni na viongozi wa jamaa za makabila ya Waisraeli.
29
Mose akawaambia, “Ikiwa Wagadi na Wareubeni, kila mwanaume aliyevaa silaha za vita, atavuka Yordani pamoja nanyi mbele za Bwana, basi wakati mtakapoishinda nchi iliyoko mbele yenu, wapeni nchi ya Gileadi kama milki yao.
30
Lakini kama hawatavuka pamoja nanyi wakiwa wamevaa silaha za vita, lazima wakubali kupokea milki yao pamoja nanyi katika nchi ya Kanaani.”
31
Wagadi na Wareubeni wakajibu, “Watumishi wako watafanya lile Bwana alilosema.
32
Tutavuka mbele za Bwana kuingia Kanaani tukiwa tumevaa silaha za vita, lakini mali tutakayoirithi itakuwa ngʼambo hii ya Yordani.”
Settings