Skip to content

Abishai

24 mistari · 3 wanafamilia

Mistari inayomtaja Abishai

  1. Basi Daudi akamuuliza Ahimeleki Mhiti, na Abishai mwana wa Seruya, nduguye Yoabu, akisema, “Ni nani atakayeshuka pamoja nami kambini kwa Sauli?” Abishai akajibu, “Nitakwenda pamoja nawe.”

  2. Hivyo Daudi na Abishai wakaenda kwenye jeshi wakati wa usiku, tazama Sauli, alikuwa amelala ndani ya kambi na mkuki wake umekitwa ardhini karibu na kichwa chake. Abneri na askari walikuwa wamelala kumzunguka Sauli.

  3. Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Sasa niruhusu nimchome mpaka ardhini kwa pigo moja la mkuki wangu; sitamchoma mara mbili.”

  4. Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize! Ni nani awezaye kutia mkono juu ya mpakwa mafuta wa Bwana na asiwe na hatia?”

  5. Wana watatu wa Seruya walikuwako huko: nao ni Yoabu, Abishai na Asaheli. Basi huyo Asaheli alikuwa na mbio kama paa.

  6. Lakini Yoabu na Abishai walimfuata Abneri, na jua lilipokuwa linatua, wakafika kwenye kilima cha Ama, karibu na Gia kwenye njia ya kuelekea kwenye nyika ya Gibeoni.

  7. (Yoabu na Abishai ndugu yake walimuua Abneri kwa sababu alikuwa amemuua Asaheli ndugu yao katika vita huko Gibeoni.)

  8. Akawaweka waliobaki chini ya uongozi wa Abishai nduguye na kuwapanga dhidi ya Waamoni.

  9. Waamoni walipoona Waaramu wanakimbia, nao wakakimbia mbele ya Abishai na kuingia ndani ya mji. Basi Yoabu akarudi kutoka kupigana na Waamoni na kufika Yerusalemu.

  10. Ndipo Abishai mwana wa Seruya akamwambia mfalme, “Kwa nini huyu mbwa mfu amlaani bwana wangu mfalme? Niruhusu nivuke nikatilie mbali kichwa chake.”

  11. Ndipo Daudi akamwambia Abishai na maafisa wake wote, “Mwanangu, yeye ambaye ametoka viunoni mwangu mwenyewe, anajaribu kuuondoa uhai wangu. Je, si zaidi sana kwa huyu Mbenyamini! Mwacheni, acha alaani, kwa maana Bwana amemwambia afanye hivyo.

  12. Daudi akatuma vikosi vya askari: theluthi moja ilikuwa chini ya amri ya Yoabu, theluthi ya pili chini ya Abishai mwana wa Seruya nduguye Yoabu, na theluthi ya tatu chini ya Itai, Mgiti. Mfalme akaviambia vikosi, “Hakika mimi mwenyewe nitakwenda pamoja nanyi.”

  13. Mfalme akawaamuru Yoabu, Abishai na Itai, “Kuweni wapole kwa kijana Absalomu kwa ajili yangu.” Vikosi vyote vikasikia mfalme akitoa amri kwa kila jemadari kumhusu Absalomu.

  14. Lakini huyo mtu akamjibu Yoabu, “Hata kama ningepimiwa shekeli 1,000 mikononi mwangu, nisingeinua mkono wangu dhidi ya mwana wa mfalme. Tukiwa tunasikia, mfalme alikuagiza wewe na Abishai pamoja na Itai, akisema, ‘Mlindeni kijana Absalomu kwa ajili yangu.’

  15. Ndipo Abishai mwana wa Seruya akasema, “Je, Shimei hapaswi kuuawa kwa ajili ya hili? Alimlaani mpakwa mafuta wa Bwana.”

  16. Daudi akamwambia Abishai, “Sasa Sheba mwana wa Bikri atatuletea madhara zaidi kuliko alivyofanya Absalomu. Wachukue watu wa bwana wako na umfuatie, la sivyo atapata mji wenye ngome na kututoroka.”

  17. Amasa hakuona upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu, naye Yoabu akamchoma nao tumboni, nayo matumbo yake yakamwagika chini. Pasipo kuchomwa mara ya pili, Amasa akafa. Basi Yoabu na Abishai nduguye wakamfuatia Sheba mwana wa Bikri.

  18. Lakini Abishai mwana wa Seruya akaja kumwokoa Daudi; akampiga huyo Mfilisti, akamwangusha chini na kumuua. Ndipo watu wakamwapia Daudi, wakisema, “Kamwe hutakwenda tena nasi vitani, ili kwamba taa ya Israeli isije ikazimwa.”

  19. Abishai ndugu yake Yoabu mwana wa Seruya ndiye alikuwa kiongozi wa hao Watatu. Aliinua mkuki wake dhidi ya watu 300 ambao aliwaua, kwa hiyo naye akawa na sifa kama hao Watatu.

  20. Dada zao walikuwa Seruya na Abigaili. Wana wa Seruya walikuwa watatu: Abishai, Yoabu na Asaheli.

  21. Abishai, ndugu yake Yoabu ndiye alikuwa kiongozi wa hao Watatu. Aliinua mkuki wake dhidi ya watu 300, ambao aliwaua, kwa hiyo naye akawa na sifa kama hao Watatu.

  22. Abishai mwana wa Seruya akawaua Waedomu 18,000 katika Bonde la Chumvi.

  23. Akawaweka wale wanajeshi wengine waliobaki chini ya amri ya Abishai ndugu yake, nao wakapangwa ili wakabiliane na Waamoni.

  24. Waamoni walipoona Waaramu wanakimbia, nao pia wakakimbia mbele ya nduguye Abishai na kuingia ndani ya mji. Basi Yoabu akarudi Yerusalemu.