Skip to content
Hesabu 32:1-19

Hesabu 32:1-19

1
Kabila la Wareubeni na Wagadi, waliokuwa na makundi makubwa ya ngʼombe, kondoo na mbuzi, waliona kuwa nchi ya Yazeri na nchi ya Gileadi ni nzuri kwa mifugo.
2
Hivyo walimjia Mose, na kuhani Eleazari na viongozi wa jumuiya, na kuwaambia,
3
“Atarothi, Diboni, Yazeri, Nimra, Heshboni, Eleale, Sebamu, Nebo na Beoni,
4
nchi ambayo Bwana ameishinda mbele ya wana wa Israeli, inafaa kwa mifugo, nao watumishi wako wana mifugo.
5
Kama tumepata kibali mbele ya macho yako, nchi hii na ipewe watumishi wako kama milki yetu. Usitufanye tuvuke Yordani.”
6
Mose akawaambia Wagadi na Wareubeni, “Je, watu wa nchi yenu watakwenda vitani wakati ninyi mmeketi hapa?
7
Kwa nini mmewakatisha Waisraeli tamaa wasivuke katika nchi ambayo Bwana amewapa?
8
Hivi ndivyo baba zenu walivyofanya wakati nilipowatuma kutoka Kadesh-Barnea kuipeleleza nchi.
9
Baada ya kufika kwenye Bonde la Eshkoli na kuitazama nchi, waliwakatisha tamaa Waisraeli wasiingie katika nchi ambayo Bwana alikuwa amewapa.
10
Siku ile hasira ya Bwana iliwaka naye akaapa kiapo hiki:
11
‘Kwa kuwa hawakunifuata kwa moyo wote, hakuna mtu yeyote mwenye miaka ishirini au zaidi ambaye alikuja kutoka Misri atakayeona nchi niliyoahidi kwa kiapo kwa Abrahamu, Isaki na Yakobo;
12
hakuna hata mmoja isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni, kwa sababu walimfuata Bwana kwa moyo wote.’
13
Hasira ya Bwana iliwaka dhidi ya Waisraeli na akawafanya watangetange katika jangwa kwa miaka arobaini, mpaka kizazi chote cha wale waliofanya maovu mbele yake kimeangamia.
14
“Nanyi mko hapa, uzao wa wenye dhambi, mkisimamia mahali pa baba zenu na mkimfanya Bwana kuwakasirikia Waisraeli hata zaidi.
15
Kama mkigeuka na mkiacha kumfuata, atawaacha tena watu hawa wote jangwani, na mtakuwa sababu ya maangamizi yao.”
16
Ndipo wakamjia Mose na kumwambia, “Tungalitaka kujenga mazizi hapa kwa ajili ya mifugo yetu na miji kwa ajili ya wanawake wetu na watoto.
17
Lakini sisi tuko tayari kuchukua silaha zetu na kutangulia mbele ya Waisraeli mpaka tutakapowaleta mahali pao. Wakati huo wanawake wetu na watoto wataishi katika miji yenye ngome, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya wenyeji wa nchi.
18
Hatutarudi nyumbani mwetu mpaka kila Mwisraeli apokee urithi wake.
19
Hatutapokea urithi wowote pamoja nao ngʼambo ya Yordani, kwa sababu urithi wetu umekuja kwetu upande wa mashariki ya Yordani.”
Settings

Reading style

Typeface

Font size 19px

Reading width 75 chars

Options