Skip to content

Mistari ya Biblia kuhusu Babylon

186 mistari · 73 vipengele

Mistari muhimu ya Biblia

Chuja kwa kitabu
  1. Mimi mwenyewe nitapigana dhidi yenu kwa mkono wangu ulionyooshwa na mkono wa nguvu, kwa hasira na ghadhabu kali na ukali mwingi.

  2. Nitawaangamiza waishio katika mji huu, watu na wanyama, nao watauawa kwa tauni ya kutisha.

  3. Baada ya hayo, nitamtia Sedekia mfalme wa Yuda, maafisa wake na watu wa mji huu ambao walinusurika tauni, upanga na njaa, mkononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, na kwa adui zao wale wanaotafuta uhai wao. Atawaua kwa upanga; hatakuwa na rehema juu yao au huruma wala kuwasikitikia,’ asema Bwana.

  4. “Zaidi ya hayo, waambie watu hawa, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Tazama, naweka mbele yenu njia ya uzima, na njia ya mauti.

  5. Yeyote atakayekaa katika mji huu atakufa kwa upanga, njaa au tauni. Lakini yeyote atakayetoka na kujisalimisha kwa Wakaldayo ambao wameuzunguka mji huu kwa jeshi, atanusurika, naye ataishi.

  6. Nimekusudia kuufanyia mji huu jambo baya, wala si jema. Utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteketeza kwa moto, asema Bwana.’

  7. “Panda Lebanoni ukapige kelele, sauti yako na isikike huko Bashani, piga kelele toka Abarimu, kwa kuwa wote waliojiunga nawe wameangamizwa.

  8. Nilikuonya wakati ulipojisikia kwamba uko salama, lakini ulisema, ‘Mimi sitasikiliza!’ Hii imekuwa kawaida yako tangu ujana wako; hujanitii mimi.

  9. Upepo utawaondoa wachungaji wako wote, na wale ulioungana nao wataenda uhamishoni. Kisha utaaibika na kufedheheka kwa sababu ya uovu wako wote.

  10. Wewe uishiye Lebanoni, wewe uliyetulia kwenye majengo ya mierezi, tazama jinsi utakavyoomboleza maumivu makali yatakapokupata, maumivu kama yale ya mwanamke mwenye utungu wa kuzaa!

  11. “Hakika kama niishivyo,” asema Bwana, “hata kama wewe, Yekonia mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, ungekuwa pete yangu ya muhuri katika mkono wangu wa kuume, bado ningekungʼoa hapo.

  12. Nitakutia mikononi mwa wale wanaotafuta uhai wako, wale unaowaogopa, yaani Nebukadneza mfalme wa Babeli na kwa Wakaldayo.

  13. Nitakutupa mbali wewe na mama aliyekuzaa mwende katika nchi nyingine, ambayo hakuna hata mmoja wenu aliyezaliwa huko, nanyi mtafia huko.

  14. nitayaita mataifa yote ya kaskazini na mtumishi wangu Nebukadneza mfalme wa Babeli,” asema Bwana. “Nitawaleta waishambulie nchi hii na wakazi wake wote, na dhidi ya mataifa yote yanayowazunguka. Nitawaangamiza kabisa na kuwafanya kitu cha kuchukiwa na kudharauliwa, na kuwa magofu daima.

  15. Nitawaondolea sauti ya shangwe na furaha, sauti ya bibi na bwana arusi, sauti ya mawe ya kusagia, na mwanga wa taa.

  16. Nchi hii yote itakuwa ukiwa na isiyofaa kitu, nayo mataifa haya yatamtumikia mfalme wa Babeli kwa miaka sabini.”

  17. Hili ndilo Bwana aliloniambia: “Tengeneza nira, ujivike shingoni mwako, uifunge kwa kamba za ngozi.

  18. Kisha utume ujumbe kwa wafalme wa Edomu, Moabu, Amoni, Tiro na Sidoni kupitia wajumbe ambao wamekuja Yerusalemu kwa Sedekia mfalme wa Yuda.

  19. Wape ujumbe kwa ajili ya mabwana zao na uwaambie: Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: ‘Waambieni hivi mabwana zenu:

  20. Kwa uwezo wangu mkuu na kwa mkono wangu ulionyooshwa nimeumba dunia na watu wake na wanyama walioko ndani yake, nami humpa yeyote inipendezavyo.

  21. Sasa nitazitia nchi zenu zote mkononi mwa mtumishi wangu Nebukadneza mfalme wa Babeli, na nitawafanya hata wanyama wa mwituni wamtumikie.

  22. Haya ndiyo maneno ya ile barua ambayo nabii Yeremia aliituma kutoka Yerusalemu kwenda kwa wazee waliobaki miongoni mwa wale waliohamishwa, na kwa makuhani, manabii na watu wengine wote ambao Nebukadneza alikuwa amewachukua kwenda uhamishoni Babeli kutoka Yerusalemu.

  23. (Hii ilikuwa ni baada ya Mfalme Yekonia na malkia mamaye, maafisa wa mahakama, viongozi wa Yuda na wa Yerusalemu, mafundi na wahunzi kwenda uhamishoni kutoka Yerusalemu.)

  24. Barua ilikabidhiwa kwa Elasa mwana wa Shafani, na kwa Gemaria mwana wa Hilkia, ambao Sedekia mfalme wa Yuda aliwatuma kwa Mfalme Nebukadneza huko Babeli. Barua yenyewe ilisema:

  25. Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, awaambialo wale wote niliowapeleka kutoka Yerusalemu kwenda uhamishoni Babeli: