Skip to content

Mistari ya Biblia kuhusu Babylon

186 mistari · 73 vipengele

Mistari muhimu ya Biblia

Chuja kwa kitabu
  1. Akawachukua watu wa Yerusalemu wote kwenda uhamishoni: yaani maafisa wote na mashujaa, watu wenye ustadi na ufundi, jumla yao watu elfu kumi. Watu maskini sana ndio tu waliobaki katika nchi.

  2. Nebukadneza akamchukua mateka Yehoyakini hadi Babeli. Pia akawachukua utumwani kutoka Yerusalemu hadi Babeli mama yake mfalme, wake zake, maafisa wake, na viongozi wote wa nchi.

  3. Mfalme wa Babeli pia akawahamishia Babeli mashujaa elfu saba, wenye nguvu na wanaofaa kupigana vita, na watu wenye ustadi na mafundi elfu moja.

  4. Hivyo katika mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia, katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli, akiwa na jeshi lake lote, alifanya vita dhidi ya Yerusalemu. Akapiga kambi nje ya mji na kuuzunguka mji pande zote.

  5. Mji ulizungukwa na jeshi mpaka mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Mfalme Sedekia.

  6. Ilipowadia siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ikazidi kuwa kali sana ndani ya mji, hadi hapakuwa na chakula kwa ajili ya watu.

  7. Kisha ukuta wa mji ukavunjwa, na jeshi lote likakimbia. Wakaondoka mjini usiku kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili karibu na bustani ya mfalme, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji. Wakakimbia kuelekea Araba.

  8. Wakaldayo walivunja vipande zile nguzo za shaba, vile vishikilio vya shaba vilivyohamishika, na ile Bahari ya shaba, ambavyo vyote vilikuwa katika Hekalu la Bwana. Hivyo wakaichukua hiyo shaba na kuipeleka Babeli.

  9. Wakachukua pia vyungu, masepetu, mikasi ya kusawazishia tambi, sahani na vyombo vyote vya shaba vilivyotumika katika huduma ya Hekalu.

  10. Jemadari wa askari walinzi wa mfalme akachukua vile vyetezo na yale mabakuli ya kunyunyizia, vitu vyote vile vilivyokuwa vimetengenezwa kwa dhahabu safi au fedha.

  11. Shaba iliyotokana na zile nguzo mbili, ile Bahari na vile vishikilio vilivyohamishika, ambavyo Solomoni alikuwa ametengeneza kwa ajili ya Hekalu la Bwana, ilikuwa na uzito usioweza kupimika.

  12. Kila nguzo ilikuwa na urefu wa dhiraa kumi na nane. Sehemu ya shaba juu ya nguzo moja ilikuwa na urefu wa dhiraa tatu na ilikuwa imepambwa kwa wavu na makomamanga ya shaba kuizunguka kote. Ile nguzo nyingine pamoja na wavu wake ilifanana na hiyo ya kwanza.

  13. Yule jemadari wa askari walinzi akawachukua kama wafungwa Seraya kuhani mkuu, kuhani Sefania aliyefuata kwa cheo, na mabawabu watatu.

  14. Miongoni mwa wale watu waliokuwa wamesalia katika mji, alimchukua afisa kiongozi wa wapiganaji, na washauri watano wa mfalme. Akamchukua pia mwandishi aliyesimamia uandikishaji wa watu wa nchi, pamoja na watu wake sitini waliopatikana ndani ya mji.

  15. Nebuzaradani jemadari akawachukua hao wote na kuwapeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribla.

  16. Huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mfalme wa Babeli akaamuru wanyongwe. Hivyo Yuda wakaenda utumwani, mbali na nchi yao.

  17. Katika mwaka wa thelathini na saba tangu Yehoyakini mfalme wa Yuda apelekwe uhamishoni, katika mwaka ule ambao Evil-Merodaki alifanyika mfalme wa Babeli, alimwacha huru Yehoyakini kutoka gerezani siku ya ishirini na saba ya mwezi wa kumi na mbili.

  18. Alizungumza naye kwa upole na kumpa kiti cha heshima zaidi kuliko wale wafalme wengine aliokuwa nao huko Babeli.

  19. Hivyo Yehoyakini akayavua mavazi yake ya mfungwa, na siku zote za maisha yake zilizobaki alikula mezani mwa mfalme.

  20. Siku kwa siku mfalme alimpa Yehoyakini posho siku zote za maisha yake.

  21. Kando ya mito ya Babeli tuliketi, tukaomboleza tulipokumbuka Sayuni.

  22. Kwenye miti ya huko tulitundika vinubi vyetu,

  23. kwa maana huko hao waliotuteka walitaka tuwaimbie nyimbo, watesi wetu walidai nyimbo za furaha; walisema, “Tuimbieni wimbo mmoja kati ya nyimbo za Sayuni!”

  24. Tutaimbaje nyimbo za Bwana, tukiwa nchi ya kigeni?

  25. Nikikusahau wewe, ee Yerusalemu, basi mkono wangu wa kuume na usahau ujuzi wake.