Skip to content
Luka 22:31-55

Luka 22:31-55

31
Yesu akasema, “Simoni, Simoni, sikiliza, Shetani ameomba kuwapepeta ninyi wote kama ngano.
32
Lakini nimekuombea wewe Simoni ili imani yako isishindwe, nawe ukiisha kunirudia, uwaimarishe ndugu zako.”
33
Petro akajibu, “Bwana, niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani na hata kifoni.”
34
Yesu akamjibu, “Ninakuambia Petro, kabla jogoo hajawika usiku wa leo, utakana mara tatu kwamba hunijui mimi.”
35
Kisha Yesu akawauliza, “Nilipowatuma bila mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu chochote?” Wakajibu, “La, hatukupungukiwa na kitu chochote.”
36
Akawaambia, “Lakini sasa, aliye na mfuko na auchukue, na aliye na mkoba vivyo hivyo. Naye asiye na upanga, auze joho lake anunue mmoja.
37
Kwa sababu, nawaambia, andiko hili lazima litimizwe juu yangu, kwamba, ‘Alihesabiwa pamoja na wakosaji’; kwa kweli yaliyoandikwa kunihusu mimi hayana budi kutimizwa.”
38
Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, tazama hapa kuna panga mbili.” Akawajibu, “Inatosha.”
39
Yesu akatoka, akaenda kwenye Mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa kawaida yake, nao wanafunzi wake wakamfuata.
40
Walipofika huko, akawaambia wanafunzi wake, “Ombeni, msije mkaingia majaribuni.”
41
Akajitenga nao kama umbali wa kutupa jiwe, akapiga magoti, akaomba
42
akisema, “Baba, kama ni mapenzi yako, niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo, bali mapenzi yako yatendeke.”
43
Malaika kutoka mbinguni akamtokea, akamtia nguvu.
44
Naye akiwa katika maumivu makuu, akaomba kwa bidii, nalo jasho lake likawa kama matone ya damu yakidondoka ardhini.
45
Baada ya kuomba, akawarudia wanafunzi wake akawakuta wamelala, wakiwa wamechoka kutokana na huzuni.
46
Naye akawauliza, “Mbona mmelala? Amkeni, mwombe ili msije mkaingia majaribuni.”
47
Yesu alipokuwa bado anazungumza, umati mkubwa wa watu ukaja. Uliongozwa na Yuda, ambaye alikuwa mmoja wa wale wanafunzi Kumi na Wawili. Akamkaribia Yesu ili ambusu.
48
Lakini Yesu akamwambia, “Yuda, je, unamsaliti Mwana wa Adamu kwa busu?”
49
Wafuasi wa Yesu walipoona yale yaliyokuwa yanakaribia kutokea, wakasema, “Bwana, tuwakatekate kwa panga zetu?”
50
Mmoja wao akampiga mtumishi wa kuhani mkuu kwa upanga, akamkata sikio la kuume.
51
Lakini Yesu akasema, “Acheni!” Akaligusa lile sikio la yule mtu na kumponya.
52
Kisha Yesu akawaambia wale viongozi wa makuhani, maafisa wa walinzi wa Hekalu, pamoja na wazee waliokuwa wamekuja kumkamata, “Mmekuja na panga na marungu, kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi?
53
Siku kwa siku nilikuwa pamoja nanyi Hekaluni lakini hamkunikamata. Lakini hii ni saa yenu, wakati giza linatawala!”
54
Kisha wakamkamata Yesu, wakamchukua, wakaenda naye mpaka nyumbani kwa kuhani mkuu. Lakini Petro akafuata kwa mbali.
55
Walipokwisha kuwasha moto katikati ya ua na kuketi pamoja, Petro naye akaketi pamoja nao.
Settings

Reading style

Typeface

Font size 19px

Reading width 75 chars

Options