Skip to content

Mistari ya Biblia kuhusu Mordecai

23 mistari · 4 vipengele

Mistari muhimu ya Biblia

  1. Basi katika mji wa ngome ya Shushani palikuwa na Myahudi wa kabila ya Benyamini, jina lake Mordekai mwana wa Yairi, mwana wa Shimei, mwana wa Kishi,

  2. ambao walichukuliwa uhamishoni kutoka Yerusalemu na Mfalme Nebukadneza wa Babeli, wakiwa miongoni mwa waliochukuliwa mateka pamoja na Mfalme Yekonia wa Yuda.

  3. Mordekai alikuwa na binamu yake msichana aliyeitwa Hadasa, ambaye alimlea kwa kuwa hakuwa na baba wala mama. Msichana huyu, ambaye pia alijulikana kwa jina la Esta, alikuwa na umbo na sura ya kupendeza, naye Mordekai alimtunza kama binti yake mwenyewe baada ya baba yake na mama yake kufariki.

  4. Wakati Mordekai alikuwa ameketi kwenye lango la mfalme, Bigthana na Tereshi, maafisa wawili wa mfalme waliokuwa walinzi wa lango, walikasirika na kupanga njama ya kumuua Mfalme Ahasuero.

  5. Lakini Mordekai aligundua hila hii na kumwambia Malkia Esta, ambaye baadaye alimwarifu mfalme, huku akimsifu Mordekai.

  6. Taarifa hiyo ilipochunguzwa na kuonekana kuwa kweli, maafisa hao wawili waliangikwa juu ya miti ya kunyongea. Haya yote yaliandikwa katika kitabu cha kumbukumbu mbele ya mfalme.

  7. Usiku ule mfalme hakupata usingizi, hivyo akaagiza aletewe kitabu cha kumbukumbu za matukio ya utawala wake, asomewe.

  8. Kitabu hicho kilikutwa na kumbukumbu kwamba Mordekai alikuwa amefichua jinsi Bigthana na Tereshi, waliokuwa maafisa wawili wa mfalme, walinzi wa lango walivyokuwa wamepanga hila ya kumuua Mfalme Ahasuero.

  9. Mfalme akauliza, “Je, ni heshima na shukrani gani Mordekai alipokea kwa ajili ya jambo hili?” Watumishi wake wakajibu, “Hakuna lolote alilofanyiwa.”

  10. Mfalme akasema, “Ni nani yuko uani?” Wakati huo huo Hamani alikuwa ameingia ua wa nje wa jumba la mfalme kusema na mfalme kuhusu kumwangika Mordekai katika mahali pa kuangikia watu alipokuwa amepajenga kwa ajili yake.

  11. Watumishi wake wakamjibu, “Hamani amesimama uani.” Mfalme akaamuru, “Mleteni ndani.”

  12. Hamani alipoingia, mfalme alimuuliza, “Afanyiwe nini mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu?” Basi Hamani akawaza moyoni mwake, “Ni nani mwingine ambaye mfalme angemheshimu kuliko mimi?”

  13. Kwa hiyo akamjibu mfalme, “Kwa mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu,

  14. aletewe joho la kifalme ambalo mfalme ameshalivaa na farasi ambaye mfalme alishampanda, ambaye amevikwa taji ya kifalme kichwani mwake.

  15. Kisha joho na farasi vikabidhiwe kwa mmojawapo wa wakuu wa mfalme anayeheshimika sana. Nao wamvike mtu yule ambaye mfalme anapenda kumheshimu, na aongozwe akiwa juu ya farasi kupitia barabara za mji, wakitangaza mbele yake, ‘Hivi ndivyo anavyofanyiwa mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu!’ ”

  16. Mfalme akamwamuru Hamani, “Nenda mara moja, chukua joho na farasi na ufanye kama vile ulivyopendekeza kwa Mordekai Myahudi, akaaye langoni mwa mfalme. Usipuuze kufanya kitu chochote ulichoshauri.”

  17. Hivyo Hamani akachukua joho na farasi. Akamvika Mordekai, na kumpandisha juu ya farasi akamtembeza katika barabara za mji akitangaza mbele yake, “Hivi ndivyo anavyofanyiwa mtu ambaye mfalme anapenda kumheshimu!”

  18. Siku ile ile Mfalme Ahasuero akampa Malkia Esta shamba la Hamani, adui wa Wayahudi. Naye Mordekai akaja mbele ya mfalme, kwa kuwa Esta alikuwa amesema jinsi anavyohusiana naye.

  19. Mfalme akaivua pete yake ya muhuri, ambayo alikuwa amemnyangʼanya Hamani, akampa Mordekai, naye Esta akamweka Mordekai juu ya shamba la Hamani.

  20. Mordekai akaondoka mbele ya mfalme akiwa amevaa mavazi ya kifalme ya buluu na nyeupe, taji kubwa la dhahabu na joho la zambarau la kitani safi. Na mji wa Shushani ukasherehekea kwa furaha.

  21. Mfalme Ahasuero alitoza ushuru katika ufalme wake wote hadi kwenye miambao yake ya mbali.

  22. Matendo yake yote ya nguvu na uwezo, pamoja na habari zote za ukuu wa Mordekai ambao mfalme alikuwa amemkuza, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Umedi na Uajemi?

  23. Mordekai Myahudi alikuwa wa pili kwa cheo kutoka Mfalme Ahasuero, naye alikuwa bora kabisa miongoni mwa Wayahudi, akipandishwa katika heshima ya juu na ndugu zake Wayahudi kwa sababu aliwatendea mema watu wake, na alizungumza kwa ajili ya ustawi wa Wayahudi wote.