God
Mistari inayomtaja God
Ee Bwana, kwa nini unatuacha twende mbali na njia zako, na kuifanya mioyo yetu migumu hata hatukukuheshimu? Rudi kwa ajili ya watumishi wako, yale makabila ambayo ni urithi wako.
Kwa maana kwa muda mfupi watu wako walimiliki mahali pako patakatifu, lakini sasa adui zetu wamepakanyaga mahali patakatifu pako.
Sisi tumekuwa kama wale ambao hujawatawala kamwe, kama wale ambao hawajaitwa kwa jina lako.
Laiti ungelipasua mbingu na kushuka chini, ili milima ingelitetemeka mbele zako!
Kama vile moto uteketezavyo vijiti na kusababisha maji kuchemka, shuka ukafanye jina lako lijulikane kwa adui zako, na kusababisha mataifa yatetemeke mbele zako!
Kwa maana ulipofanya mambo ya kutisha ambayo hatukuyatazamia, ulishuka, nayo milima ikatetemeka mbele zako.
Tangu nyakati za zamani hakuna yeyote aliyesikia, hakuna sikio lililotambua, hakuna jicho lililomwona Mungu mwingine ila wewe, anayetenda mambo kwa ajili ya wale wamngojeao.
Uliwasaidia watu wale watendao yaliyo haki kwa furaha, wale wazikumbukao njia zako. Lakini wakati tulipoendelea kutenda dhambi kinyume na njia zako, ulikasirika. Tutawezaje basi kuokolewa?
Hakuna yeyote anayeliitia jina lako wala anayejitahidi kukushika, kwa kuwa umetuficha uso wako na kutuacha tudhoofike kwa sababu ya dhambi zetu.
Lakini, Ee Bwana, wewe ndiwe Baba yetu. Sisi ni udongo, wewe ndiye mfinyanzi; sisi sote tu kazi ya mkono wako.
Ee Bwana, usikasirike kupita kiasi, usizikumbuke dhambi zetu milele. Ee Bwana, utuangalie, twakuomba, kwa kuwa sisi sote tu watu wako.
Ee Bwana, baada ya haya yote, utajizuia? Je, utanyamaza kimya na kutuadhibu kupita kiasi?
“Nilijifunua kwa watu wale ambao hawakuniulizia. Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta. Kwa taifa lile ambalo halikuliita Jina langu, nilisema, ‘Niko hapa, niko hapa.’
Mchana kutwa nimeinyoosha mikono yangu kwa watu wakaidi, wanaokwenda katika njia ambazo si nzuri, wafuatao mawazo yao wenyewe:
taifa ambalo daima hunikasirisha machoni pangu, wakitoa dhabihu katika bustani na kufukiza uvumba juu ya madhabahu za matofali;
wasemao, ‘Kaa mbali; usinikaribie, kwa maana mimi ni mtakatifu mno kwako!’ Watu wa aina hiyo ni moshi katika pua zangu, ni moto uwakao mchana kutwa.
“Tazama, jambo hili hubakia limeandikwa mbele zangu: sitanyamaza, bali nitalipiza kwa ukamilifu; nitalipiza mapajani mwao:
dhambi zenu na dhambi za baba zenu,” asema Bwana. “Kwa sababu walitoa dhabihu za kuteketezwa juu ya milima na kunichokoza mimi juu ya vilima, nitawapimia mapajani mwao malipo makamilifu kwa matendo yao ya zamani.”
Hili ndilo asemalo Bwana: “Kama vile divai mpya ingali bado inapatikana katika kishada cha zabibu, nao watu husema, ‘Usikiharibu, kwa kuwa bado kuna kitu kizuri ndani yake,’ hivyo ndivyo nitakavyofanya kwa ajili ya watumishi wangu; sitawaangamiza wote.
Nitawaleta wazao kutoka kwa Yakobo, na kutoka kwa Yuda wale watakaomiliki milima yangu, nao watu wangu wateule watairithi, nako huko wataishi watumishi wangu.
Sharoni itakuwa malisho kwa ajili ya makundi ya kondoo, na Bonde la Akori mahali pa kupumzikia kwa makundi ya ngʼombe, kwa ajili ya watu wangu wanaonitafuta.
“Bali kwenu ninyi mnaomwacha Bwana na kuusahau mlima wangu mtakatifu, ninyi mnaoandaa meza kwa ajili ya Bahati, na kujaza mabakuli ya mvinyo uliochanganywa kwa ajili ya Ajali,
nitawaagiza mfe kwa upanga, nanyi nyote mtainama chini ili kuchinjwa; kwa kuwa niliwaita lakini hamkuitika, nilisema lakini hamkusikiliza. Mlitenda maovu machoni pangu, nanyi mkachagua mambo yale yanayonichukiza.”
Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: “Watumishi wangu watakula, lakini ninyi mtaona njaa; watumishi wangu watakunywa lakini ninyi mtaona kiu; watumishi wangu watafurahi, lakini ninyi mtaona haya.
Watumishi wangu wataimba kwa furaha ya mioyo yao, lakini ninyi mtalia kutokana na uchungu wa moyoni, na kupiga yowe kwa sababu ya uchungu wa roho zenu.