Mathayo 22:23-46
23
Siku hiyo hiyo Masadukayo, wale wasemao kwamba hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu na kumuuliza swali, wakisema,
24
“Mwalimu, Mose alisema, ‘Kama mtu akifa bila kuwa na watoto, ndugu yake inampasa amwoe huyo mjane ili ampatie watoto huyo nduguye aliyekufa.’
25
Basi palikuwa na ndugu saba miongoni mwetu. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa, na kwa kuwa hakuwa na watoto, akamwachia nduguye yule mjane.
26
Ikatokea vivyo hivyo kwa yule ndugu wa pili, na wa tatu, hadi wote saba.
27
Hatimaye, yule mwanamke naye akafa.
28
Sasa basi, siku ya ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba, kwa kuwa wote walikuwa wamemwoa huyo mwanamke?”
29
Yesu akawajibu, “Mwapotoka kwa sababu hamjui Maandiko wala uweza wa Mungu.
30
Wakati wa ufufuo, watu hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni.
31
Lakini kuhusu ufufuo wa wafu, hamjasoma kile Mungu alichowaambia, kwamba,
32
‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo’? Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.”
33
Ule umati wa watu uliposikia hayo, ulishangaa sana kwa mafundisho yake.
34
Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, Mafarisayo wakakusanyika pamoja.
35
Mmoja wao, mtaalamu wa sheria, akamuuliza swali ili kumjaribu, akisema,
36
“Mwalimu, ni amri ipi katika Sheria iliyo kuu kuliko zote?”
37
Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’
38
Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza.
39
Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’
40
Amri hizi mbili ndizo msingi wa Sheria na Manabii.”
41
Wakati Mafarisayo walikuwa wamekusanyika pamoja, Yesu akawauliza,
42
“Mnaonaje kuhusu Kristo?Yeye ni mwana wa nani?” Wakamjibu, “Yeye ni mwana wa Daudi.”
43
Akawaambia, “Inakuwaje basi kwamba Daudi, akinena kwa kuongozwa na Roho, anamwita Kristo ‘Bwana’? Kwa maana asema,
44
“ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: “Keti mkono wangu wa kuume, hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.” ’
45
Kama basi Daudi anamwita yeye ‘Bwana,’ awezaje kuwa mwanawe?”
46
Hakuna mtu aliyeweza kumjibu Yesu neno. Tena tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu kumuuliza tena maswali.
Settings