Ezekieli 16:35-52
35
“ ‘Kwa hiyo, wewe kahaba, sikia neno la Bwana!
36
Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa kuwa umemwaga tamaa zako na kuonyesha uchi wako katika uzinzi wako kwa wapenzi wako na kwa sababu ya sanamu zako zote za machukizo na kwa sababu uliwapa damu ya watoto wako,
37
kwa hiyo nitawakusanya wapenzi wako wote, wale ambao ulijifurahisha nao, wale uliowapenda na wale uliowachukia pia. Nitawakusanya wote dhidi yako kutoka pande zote na nitakuvua nguo mbele yao, nao wataona uchi wako wote.
38
Nitakuhukumia adhabu wanayopewa wanawake wafanyao uasherati na hao wamwagao damu, nitaleta juu yenu kisasi cha damu cha ghadhabu yangu na wivu wa hasira yangu.
39
Kisha nitakutia mikononi mwa wapenzi wako, nao watabomoa majukwaa yako na kuharibu mahali pako pa fahari pa ibada ya miungu. Watakuvua nguo zako na kuchukua vito vyako vya thamani na kukuacha uchi na bila kitu.
40
Wataleta kundi la watu dhidi yako, watakaokupiga kwa mawe na kukukatakata vipande vipande kwa panga zao.
41
Watachoma nyumba zako na kutekeleza adhabu juu yako machoni pa wanawake wengi. Nitakomesha ukahaba wako, nawe hutawalipa tena wapenzi wako.
42
Ndipo ghadhabu yangu dhidi yako itakapopungua na wivu wa hasira yangu utaondoka kwako. Nitatulia wala sitakasirika tena.
43
“ ‘Kwa sababu hukuzikumbuka siku za ujana wako, lakini ulinikasirisha kwa mambo haya yote, hakika nitaleta juu ya kichwa chako yale uliyotenda, asema Bwana Mwenyezi. Je hukuongeza uasherati juu ya matendo yako yote ya kuchukiza?
44
“ ‘Kila mtu atumiaye maneno ya mithali hii, atayatumia juu yako: “Alivyo mama, ndivyo alivyo bintiye.”
45
Wewe ni binti halisi wa mama yako, ambaye alimchukia kabisa mume wake na watoto wake, tena wewe ni dada halisi wa dada zako, waliowachukia kabisa waume zao na watoto wao. Mama yako alikuwa Mhiti na baba yako alikuwa Mwamori.
46
Dada yako mkubwa alikuwa Samaria, aliyeishi upande wako wa kaskazini na binti zake, pamoja na dada yake, naye dada yako mdogo, aliyeishi kusini yako pamoja na binti zake, alikuwa Sodoma.
47
Hukuziendea njia zao tu na kuiga matendo yao ya kuchukiza, bali kwa muda mfupi katika njia zako zote uliharibika tabia zaidi kuliko wao.
48
Hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, dada yako Sodoma pamoja na binti zake, kamwe hawakufanya yale ambayo wewe na binti zako mmefanya.
49
“ ‘Sasa hii ilikuwa ndiyo dhambi ya dada yako Sodoma: yeye na binti zake walikuwa na majivuno, walafi na wazembe, hawakuwasaidia maskini na wahitaji.
50
Walijivuna na kufanya mambo ya machukizo sana mbele zangu. Kwa hiyo niliwakatilia mbali nami kama mlivyoona.
51
Samaria hakufanya hata nusu ya dhambi ulizofanya. Wewe umefanya mambo mengi sana ya kuchukiza kuwaliko wao, nawe umewafanya dada zako waonekane kama wenye haki kwa ajili ya mambo haya yote uliyoyafanya.
52
Chukua aibu yako, kwa kuwa umefanya uovu wa dada zako uwe si kitu, nao waonekane kama wenye haki. Kwa kuwa dhambi zako zilikuwa mbaya zaidi kuliko zao, wameonekana wenye haki zaidi kuliko wewe. Kwa hiyo basi, chukua aibu yako, kwa kuwa umewafanya dada zako waonekane wenye haki.
Settings