Ezekieli 16:15-34
15
“ ‘Lakini ulitumainia uzuri wako na kutumia umaarufu wako kuwa kahaba. Ulifanya uzinzi kwa kila mtu aliyepita, uzuri wako ukawa kwa ajili yake.
16
Ulichukua baadhi ya mavazi yako ukayatumia kupamba mahali pako pa juu pa kuabudia miungu, mahali ambapo ulifanyia ukahaba wako. Mambo ya namna hiyo hayastahili kutendeka wala kamwe kutokea.
17
Pia ulichukua vito vizuri nilivyokupa, vito vilivyotengenezwa kwa dhahabu yangu na fedha yangu, ukajitengenezea navyo sanamu za kiume na ukafanya ukahaba nazo.
18
Ukayachukua mavazi yako niliyokupa yaliyotariziwa na ukazivalisha hizo sanamu, ukatoa mbele ya hizo sanamu mafuta yangu na uvumba wangu.
19
Pia chakula changu nilichokupa ili ule: unga laini, mafuta ya zeituni na asali, ulivitoa mbele yao kuwa uvumba wa harufu nzuri. Hayo ndiyo yaliyotokea, asema Bwana Mwenyezi.
20
“ ‘Nawe uliwachukua wanao na binti zako ulionizalia mimi na kuwatoa kafara kuwa chakula kwa sanamu. Je, ukahaba wako haukukutosha?
21
Uliwachinja watoto wangu na kuwatoa kafara kwa sanamu.
22
Katika matendo yako yote ya machukizo, pamoja na ukahaba wako hukukumbuka siku za ujana wako, wakati ulipokuwa uchi kabisa bila kitu chochote, ulipokuwa ukigaagaa kwenye damu yako.
23
“ ‘Ole! Ole wako! Asema Bwana Mwenyezi. Pamoja na maovu yako yote mengine,
24
Ukajijengea jukwaa na kujifanyia mahali pa fahari pa ibada za miungu kwenye kila uwanja wa mikutano.
25
Katika kila mwanzo wa barabara ulijenga mahali pa fahari pa ibada za miungu na kuaibisha uzuri wako, ukiutoa mwili wako kwa kuzidisha uzinzi kwa kila apitaye.
26
Ulifanya ukahaba wako na Wamisri, jirani zako waliojaa tamaa, ukaichochea hasira yangu kwa kuongezeka kwa uzinzi wako.
27
Hivyo nilinyoosha mkono wangu dhidi yako na kuipunguza nchi yako, nikakutia kwenye ulafi wa adui zako, binti za Wafilisti, walioshtushwa na tabia yako ya uasherati.
28
Ulifanya ukahaba na Waashuru pia, kwa kuwa hukuridhika, hata baada ya hayo, ukawa bado hukutosheleka.
29
Ndipo ukaongeza uzinzi wako kwa Wakaldayo nchi ya wafanyabiashara, hata katika hili hukutosheka.
30
“ ‘Tazama jinsi ulivyo na dhamiri dhaifu, asema Bwana Mwenyezi, unapofanya mambo haya yote, ukifanya kama kahaba asiyekuwa na aibu!
31
Unapojenga jukwaa lako kila mwanzo wa barabara na kufanyiza mahali pa fahari pa ibada za miungu katika kila kiwanja cha wazi, lakini hukuwa kama kahaba, kwa sababu ulidharau malipo.
32
“ ‘Wewe mke mzinzi! Unapenda wageni, kuliko mume wako mwenyewe.
33
Kila kahaba hupokea malipo, lakini wewe hutoa zawadi kwa wapenzi wako wote, ukiwahonga ili waje kwako kutoka kila mahali kwa ajili ya ukahaba wako.
34
Kwa hiyo wewe ulikuwa tofauti na wanawake wengine kwenye ukahaba wako, hakuna aliyekutongoza ili kuzini naye, wewe ndiye uliyelipa wakati hakuna malipo uliyolipwa wewe. Wewe ulikuwa tofauti.
Settings