Skip to content
2 Nyakati 25:14-28

2 Nyakati 25:14-28

14
Amazia aliporudi kutoka kuwachinja Waedomu, alileta pia kutoka huko miungu ya watu wa Seiri. Akaisimamisha kama miungu yake mwenyewe, akaisujudia na kuitolea kafara za kuteketezwa.
15
Hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Amazia, naye akamtuma nabii kwake, ambaye alisema: “Kwa nini unauliza kwa miungu ya hawa watu, ambayo haikuweza kuwaokoa watu wake wenyewe kutoka mkononi mwako?”
16
Wakati nabii alipokuwa angali anazungumza, mfalme akamwambia, “Je, wewe tumekuchagua kuwa mshauri wa mfalme? Nyamaza, ya nini uuawe?” Hivyo nabii akanyamaza lakini akasema, “Najua kuwa Mungu ameazimia kukuangamiza kwa sababu umefanya jambo hili na hukusikiliza shauri langu.”
17
Baada ya Amazia mfalme wa Yuda kushauriana na washauri wake akatuma ujumbe kwa Yehoashi, mwana wa Yehoahazi mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli kusema: “Njoo tukabiliane uso kwa uso.”
18
Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli akamjibu Amazia mfalme wa Yuda, “Mbaruti uliokuwa Lebanoni ulituma ujumbe kwa mwerezi uliokuwa Lebanoni, ‘Mtoe binti yako aolewe na mwanangu.’ Kisha mnyama wa mwituni aliyekuwa Lebanoni akaja na kuukanyaga ule mbaruti.
19
Wewe unasema moyoni mwako kwamba umemshinda Edomu, nawe sasa unajigamba na kujivuna. Lakini kaa nyumbani kwako! Kwa nini utafute matatizo na kujiletea anguko lako mwenyewe na la Yuda pia?”
20
Hata hivyo, Amazia hakutaka kusikia, kwa kuwa Mungu alifanya hivyo ili awatie mikononi mwa Yehoashi, kwa sababu waliitafuta miungu ya Edomu.
21
Hivyo Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea kuwashambulia. Yeye na Amazia mfalme wa Yuda wakakabiliana uso kwa uso huko Beth-Shemeshi katika Yuda.
22
Yuda ikashindwa na Israeli na kila mtu akakimbilia nyumbani kwake.
23
Yehoashi mfalme wa Israeli akamteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-Shemeshi. Kisha Yehoashi akamleta Yerusalemu na kuubomoa ukuta wa Yerusalemu kuanzia lango la Efraimu hadi Lango la Pembeni, sehemu yenye urefu wa kama dhiraa 400.
24
Akachukua dhahabu yote, fedha na vyombo vyote vilivyopatikana katika Hekalu la Mungu, ambavyo vilikuwa chini ya uangalizi wa Obed-Edomu, pamoja na hazina za jumba la mfalme na mateka, kisha akarudi Samaria.
25
Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na mitano baada ya kifo cha Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli.
26
Kwa habari ya matukio mengine katika utawala wa Amazia, kuanzia mwanzo hadi mwisho, je, hayakuandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na wa Israeli?
27
Kuanzia wakati ule Amazia alipogeuka na kuacha kumfuata Bwana walifanya shauri baya dhidi yake huko Yerusalemu naye akakimbilia Lakishi, lakini wakawatuma watu wamfuatilie huko Lakishi nao wakamuulia huko.
28
Akarudishwa kwa farasi na akazikwa pamoja na baba zake katika Mji wa Yuda.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options