2 Nyakati 25:17-24
17
Baada ya Amazia mfalme wa Yuda kushauriana na washauri wake akatuma ujumbe kwa Yehoashi, mwana wa Yehoahazi mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli kusema: “Njoo tukabiliane uso kwa uso.”
18
Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli akamjibu Amazia mfalme wa Yuda, “Mbaruti uliokuwa Lebanoni ulituma ujumbe kwa mwerezi uliokuwa Lebanoni, ‘Mtoe binti yako aolewe na mwanangu.’ Kisha mnyama wa mwituni aliyekuwa Lebanoni akaja na kuukanyaga ule mbaruti.
19
Wewe unasema moyoni mwako kwamba umemshinda Edomu, nawe sasa unajigamba na kujivuna. Lakini kaa nyumbani kwako! Kwa nini utafute matatizo na kujiletea anguko lako mwenyewe na la Yuda pia?”
20
Hata hivyo, Amazia hakutaka kusikia, kwa kuwa Mungu alifanya hivyo ili awatie mikononi mwa Yehoashi, kwa sababu waliitafuta miungu ya Edomu.
21
Hivyo Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea kuwashambulia. Yeye na Amazia mfalme wa Yuda wakakabiliana uso kwa uso huko Beth-Shemeshi katika Yuda.
22
Yuda ikashindwa na Israeli na kila mtu akakimbilia nyumbani kwake.
23
Yehoashi mfalme wa Israeli akamteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-Shemeshi. Kisha Yehoashi akamleta Yerusalemu na kuubomoa ukuta wa Yerusalemu kuanzia lango la Efraimu hadi Lango la Pembeni, sehemu yenye urefu wa kama dhiraa 400.
24
Akachukua dhahabu yote, fedha na vyombo vyote vilivyopatikana katika Hekalu la Mungu, ambavyo vilikuwa chini ya uangalizi wa Obed-Edomu, pamoja na hazina za jumba la mfalme na mateka, kisha akarudi Samaria.
Settings