1 Samweli 25:27-44
27
Nayo zawadi hii ambayo mtumishi wako amemletea bwana wangu, wapewe watu wanaofuatana nawe.
28
Tafadhali samehe kosa la mtumishi wako, kwa kuwa Bwana kwa hakika ataifanya imara nyumba ya ufalme kwa bwana wangu, kwa sababu anapigana vita vya Bwana.
29
Hata ingawa yuko mtu anayekufuatia kuuondoa uhai wako, usiruhusu baya lolote kuonekana kwako siku zote za maisha yako, uhai wa bwana wangu utafungwa salama kwenye furushi la walio hai na Bwana Mungu wako. Lakini uhai wa adui zako atavurumishwa kama vile jiwe kutoka kwenye kombeo.
30
Bwana atakapokuwa ameshamtendea bwana wangu kila kitu chema alichoahidi kumhusu yeye na kumweka kuwa kiongozi wa Israeli,
31
bwana wangu hatakuwa na dhamiri inayolemewa na mzigo kwa kumwaga damu kusiko na sababu, au kujilipizia kisasi yeye mwenyewe. Bwana atakapomletea bwana wangu mafanikio, umkumbuke mtumishi wako.”
32
Daudi akamwambia Abigaili, “Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli aliyekutuma kunilaki leo.
33
Ubarikiwe kwa uamuzi wako mzuri na kwa kunizuia nisimwage damu leo na kulipiza kisasi kwa mikono yangu.
34
La sivyo, hakika kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye amenizuia nisiwadhuru, kama usingekuja haraka kunilaki, hakuna hata mwanaume mmoja wa Nabali angeachwa hai kufikia mapambazuko.”
35
Ndipo Daudi akapokea kutoka mkononi mwake kile alichokuwa amemletea, naye akasema, “Nenda nyumbani kwako kwa amani; nimesikia maneno yako na kukujalia ombi lako.”
36
Abigaili alipokwenda kwa Nabali, alikuwa ndani ya nyumba yake akifanya karamu kama ile ya mfalme. Naye alikuwa ana furaha nyingi, akiwa amelewa sana. Kwa hiyo Abigaili hakumwambia mumewe kitu chochote mpaka asubuhi yake.
37
Basi asubuhi, Nabali alipokuwa amelevuka, mkewe akamwambia mambo yote, nao moyo wake ukazimia, akawa kama jiwe.
38
Baada ya siku kumi, Bwana akampiga Nabali, naye akafa.
39
Daudi aliposikia kwamba Nabali amekufa, akasema, “Ahimidiwe Bwana, ambaye amenitetea shauri langu dhidi ya Nabali kwa kuwa alinitendea kwa dharau. Amemzuia mtumishi wake asitende mabaya na Bwana ameuleta ubaya wa Nabali juu ya kichwa chake mwenyewe.” Kisha Daudi akatuma ujumbe kwa Abigaili kumwomba awe mke wake.
40
Watumishi wa Daudi wakaenda mpaka Karmeli na kumwambia Abigaili, wakisema, “Daudi ametutuma kwako kukuchukua uwe mkewe.”
41
Akainama chini uso wake mpaka ardhini, akasema, “Mjakazi wako yuko hapa, tayari kuwatumikia na kuwanawisha miguu watumishi wa bwana wangu.”
42
Abigaili akainuka kwa haraka, akapanda punda wake, akihudumiwa na wajakazi wake watano, akaenda pamoja na wajumbe wa Daudi, naye akawa mkewe.
43
Pia Daudi alikuwa amemwoa Ahinoamu wa Yezreeli, wote wawili wakawa wake zake.
44
Lakini Sauli alikuwa amemwoza Mikali binti yake, aliyekuwa mkewe Daudi, kwa Palti mwana wa Laishi, kutoka Galimu.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings