Skip to content

Mistari ya Biblia kuhusu Ruth

48 mistari · 8 vipengele

Mistari muhimu ya Biblia

  1. Bwana na akulipe kwa yale uliyoyatenda. Ubarikiwe kwa wingi na Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye umekimbilia mabawani mwake.”

  2. Kisha Ruthu akasema, “Naomba niendelee kupata kibali machoni pako, bwana wangu. Kwa maana umenifariji na umezungumza kwa ukarimu na mjakazi wako, hata ingawa mimi si bora kama mmoja wa watumishi wako wa kike.”

  3. Wakati wa chakula, Boazi akamwambia Ruthu, “Karibia hapa. Kula mkate na uchovye ndani ya siki.” Alipoketi pamoja na wavunaji, akampa nafaka zilizookwa. Akala kiasi alichotaka na kusaza.

  4. Alipoinuka ili kuokota mabaki ya nafaka, Boazi akawaagiza watu wake, “Hata kama atakusanya kati ya miganda, msimzuie.

  5. Badala yake, toeni masuke katika miganda, mwachieni ayaokote, na msimkemee.”

  6. Basi Ruthu akaokota masazo shambani hata jioni. Akatwanga ile shayiri aliyokusanya, ikajaa efa moja.

  7. Kisha Naomi akamwambia mkwewe, “Binti yangu, je, nisingelikutafutia pumziko ambako utatunzika vyema?

  8. Je, Boazi, ambaye umekuwa pamoja na watumishi wake wasichana, si jamaa yetu wa karibu? Usiku wa leo atakuwa anapepeta ngano kwenye sakafu ya kupuria.

  9. Basi oga na ukajipake marashi, ujivalie nguo zako nzuri. Kisha uende kwenye sakafu ya kupuria, lakini angalia asijue kwamba upo pale mpaka atakapomaliza kula na kunywa.

  10. Atakapokwenda kulala, angalia mahali atakapolala. Kisha uende ufunue miguu yake, ulale. Naye atakuambia utakalofanya.”

  11. Ruthu akajibu, “Lolote usemalo nitatenda.”

  12. Basi akashuka mpaka kwenye sakafu ya kupuria, akafanya kila kitu mama mkwe wake alichomwambia kufanya.

  13. Wakati Boazi alipomaliza kula na kunywa, naye akawa amejawa na furaha, alikwenda kulala mwisho wa lundo la nafaka. Ruthu akanyemelea polepole, akafunua miguu yake, na akalala.

  14. Usiku wa manane, kitu kilimshtua Boazi, akajigeuza, akagundua yupo mwanamke amelala miguuni pake.

  15. Akauliza, “Wewe ni nani?” Akajibu, “Ni mimi Ruthu, mjakazi wako. Uitande nguo yako juu yangu, kwa sababu wewe ndiwe jamaa wa karibu wa kutukomboa.”

  16. Pia akamwambia, “Leta shela yako uliyoivaa, uitandaze.” Naye alipoitandaza, akamimina vipimo sita vya shayiri, akamtwika. Kisha Ruthu akarudi zake mjini.

  17. Kisha Boazi akawatangazia wazee na watu wote waliokuwepo, “Leo ninyi ni mashahidi kwamba mimi nimenunua kutoka kwa Naomi yote yaliyokuwa mali ya Elimeleki, Kilioni na Maloni.

  18. Nimemchukua pia Ruthu, Mmoabu, mjane wa Maloni, awe mke wangu, ili kuendeleza jina la marehemu pamoja na mali zake, ili jina lake marehemu lisitoweke miongoni mwa jamaa yake, wala katika kumbukumbu za mji wake. Leo hivi ninyi ni mashahidi!”

  19. Kisha wazee pamoja na watu wote waliokuwa langoni wakasema, “Sisi ni mashahidi. Bwana na amfanye mwanamke huyu aingiaye nyumbani mwako kuwa kama Raheli na kama Lea, wale wanawake wawili ambao pamoja waliijenga nyumba ya Israeli. Nawe ufanikiwe katika Efrathi na uwe mashuhuri katika Bethlehemu.

  20. Kupitia kwa watoto ambao Bwana atakupa kutokana na huyu mwanamwali, jamaa yako na ifanane na ya Peresi, ambaye Tamari alimzalia Yuda.”

  21. Basi Boazi akamwoa Ruthu, naye akawa mke wake. Alipoingia kwake, Bwana akamjalia Ruthu, naye akapata mimba, akamzaa mtoto wa kiume.

  22. Salmoni akamzaa Boazi, Boazi akamzaa Obedi,

  23. Obedi akamzaa Yese, na Yese akamzaa Daudi.