Marko 12:13-34
13
Baadaye wakawatuma baadhi ya Mafarisayo na Maherode ili kwenda kumtega Yesu katika yale anayosema.
14
Wakamjia, wakamwambia, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu. Wewe huyumbishwi na wanadamu, kwa kuwa huna upendeleo. Lakini wewe huifundisha njia ya Mungu katika kweli. Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la?
15
Je, tulipe kodi au tusilipe?” Lakini Yesu alijua unafiki wao. Akawauliza “Mbona mnajaribu kunitega? Nileteeni hiyo dinariniione.”
16
Wakamletea hiyo sarafu. Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?” Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.”
17
Ndipo Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.” Nao wakamstaajabia sana.
18
Kisha Masadukayo, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu,
19
wakasema, “Mwalimu, Mose alituandikia kuwa kama ndugu wa mtu akifa na kumwacha mkewe bila mtoto, basi huyo mtu inampasa amwoe huyo mjane ili amzalie ndugu yake watoto.
20
Basi palikuwepo ndugu saba. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa pasipo kuwa na mtoto yeyote.
21
Wa pili akamwoa yule mjane, lakini naye akafa bila kuacha mtoto yeyote. Ikawa vivyo hivyo kwa yule wa tatu.
22
Hakuna hata mmojawapo wa hao ndugu wote saba aliyeacha mtoto. Hatimaye yule mwanamke naye akafa.
23
Kwa hiyo wakati wa ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani, maana aliolewa na ndugu wote saba?”
24
Yesu akawajibu, “Je, hampotoki kwa sababu hamfahamu Maandiko wala uweza wa Mungu?
25
Wafu watakapofufuka, hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni.
26
Basi kuhusu wafu kufufuliwa, je hamjasoma katika Kitabu cha Mose jinsi Mungu alivyosema na Mose kutoka kile kichaka akisema, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo?’
27
Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai. Kwa hiyo mmekosea kabisa.”
28
Mwalimu mmoja wa sheria akaja, akawasikia wakijadiliana. Akiona kwamba Yesu amewajibu vyema, naye akamuuliza, “Katika amri zote, ni ipi iliyo kuu?”
29
Yesu akajibu, “Amri iliyo kuu ndiyo hii: ‘Sikia ee Israeli. Bwana Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja.
30
Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.’
31
Ya pili ndiyo hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.”
32
Yule mwalimu wa sheria akamwambia Yesu, “Mwalimu, umejibu vyema kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye.
33
Kumpenda Mungu kwa moyo wote na kwa akili zote na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama mtu anavyojipenda mwenyewe ni bora zaidi kuliko kutoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu zote.”
34
Yesu alipoona kwamba amejibu kwa busara, akamwambia, “Wewe hauko mbali na Ufalme wa Mungu.” Tangu wakati huo, hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumuuliza maswali tena.
Settings