Skip to content
Walawi 25:29-53

Walawi 25:29-53

29
“ ‘Ikiwa mtu atauza nyumba iliyo ndani ya mji uliozungukwa kwa ukuta, yeye anayo haki ya kuikomboa mwaka mzima baada ya mauzo ya hiyo nyumba. Wakati huo anaweza kuikomboa.
30
Ikiwa haikukombolewa kabla ya mwaka mmoja kamili kupita, nyumba iliyo ndani ya mji uliozungukwa kwa ukuta itakuwa mali ya kudumu ya mnunuzi na wazao wake. Haitarudishwa mwaka wa Yubile.
31
Lakini nyumba zilizo vijijini bila ya kuwa na kuta zilizozizunguka zitahesabiwa kama mashamba. Zinaweza kukombolewa, nazo zirudishwe katika mwaka wa Yubile.
32
“ ‘Walawi siku zote wana haki ya kukomboa nyumba zao katika miji ya Walawi wanayoimiliki.
33
Kwa hiyo mali ya Mlawi inaweza kukombolewa, yaani nyumba iliyouzwa katika mji wowote wanaoushikilia itarudishwa mwaka wa Yubile, kwa sababu nyumba zilizo katika miji ya Walawi ni mali yao miongoni mwa Waisraeli.
34
Lakini nchi ya malisho iliyo mali ya miji yao kamwe isiuzwe, ni milki yao ya kudumu.
35
“ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini, naye akashindwa kujitegemeza mwenyewe katikati yako, msaidie kama vile ambavyo ungelimsaidia mgeni au kama mkazi wa muda, ili aweze kuendelea kuishi katikati yako.
36
Usichukue riba wala faida yoyote kutoka kwake, bali utamwogopa Mungu wako, ili mzawa wa nchi yako aweze kuendelea kuishi katikati yako.
37
Usimkopeshe fedha ili alipe na riba, wala usimuuzie chakula kwa faida.
38
Mimi ndimi Bwana Mungu wako, niliyekuleta kutoka nchi ya Misri nikupe nchi ya Kanaani, nami niwe Mungu wako.
39
“ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini katikati yako, naye akajiuza kwako, usimfanye atumike kama mtumwa.
40
Atatendewa kama mfanyakazi aliyeajiriwa, au kama mkazi wa muda katikati yako, naye atatumika mpaka Mwaka wa Yubile.
41
Ndipo yeye na watoto wake wataachiwa, naye atarudi kwa watu wa ukoo wake, na kwenye mali ya baba zake.
42
Kwa sababu Waisraeli ni watumishi wangu niliowaleta kutoka nchi ya Misri, kamwe wasiuzwe kama watumwa.
43
Usiwatawale kwa ukatili, lakini utamcha Mungu wako.
44
“ ‘Watumwa wako wa kiume na wa kike watatoka katika mataifa yanayokuzunguka; kutoka kwao waweza kununua watumwa.
45
Pia waweza kununua baadhi ya wakazi wa muda wanaoishi katikati yako, na jamaa ya koo zao waliozaliwa katika nchi yako, nao watakuwa mali yako.
46
Hao waweza kuwarithisha watoto wako kuwa urithi wao, na wanaweza kuwafanya watumwa maisha yao yote, lakini usiwatawale ndugu zako Waisraeli kwa ukatili.
47
“ ‘Ikiwa mgeni au mkazi wa muda katikati yako atakuwa tajiri, na mmoja wa wazawa wa nchi yako akawa maskini, naye akajiuza kwa yule mgeni anayeishi katikati yako, au kwa mmoja wa jamaa wa koo za wageni,
48
anayo haki ya kukombolewa baada ya kujiuza. Mmoja wa jamaa zake aweza kumkomboa:
49
Mjomba wake, au binamu yake, au yeyote aliye ndugu wa damu katika ukoo wake aweza kumkomboa. Au ikiwa atafanikiwa, anaweza kujikomboa mwenyewe.
50
Yeye na huyo aliyemnunua watahesabu muda kuanzia mwaka aliojiuza hadi Mwaka wa Yubile. Mahali pa kuanzia bei ya kuachiwa kwake itakadiriwa kwa ujira unaolipwa mfanyakazi aliyeajiriwa kwa idadi ya hiyo miaka.
51
Ikiwa imebaki miaka mingi, ni lazima atalipia ukombozi wake fungu kubwa la bei iliyolipwa kumnunua yeye.
52
Ikiwa miaka iliyobaki ni michache kufikia Mwaka wa Yubile, atafanya hesabu yake, naye atalipa malipo yanayostahili kwa ajili ya ukombozi wake.
53
Atatendewa kama mtu wa kuajiriwa mwaka hadi mwaka; lazima uone kwamba yule aliyemnunua hamtawali kwa ukatili.

Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.

Settings

Reading style

Typeface

Font size 19px

Reading width 75 chars

Options