Waamuzi 18:1-16
1
Katika siku hizo Israeli walikuwa hawana mfalme. Katika siku hizo kabila la Wadani walikuwa wanatafuta mahali pao wenyewe pa kuishi, kwa sababu walikuwa hawajafika kwenye urithi wao miongoni mwa makabila ya Israeli.
2
Hivyo Wadani wakatuma mashujaa watano kutoka Sora na Eshtaoli ili kupeleleza nchi na kuichunguza. Hawa watu waliwakilisha koo zao zote. Waliwaambia, “Nendeni mkaichunguze hiyo nchi.” Watu hao wakaingia katika nchi ya vilima ya Efraimu, nao wakafika nyumba ya Mika, ambako walilala usiku huo.
3
Walipofika karibu na nyumba ya Mika, waliitambua sauti ya yule kijana Mlawi; hivyo wakaingia humo na kumuuliza, “Ni nani aliyekuleta hapa? Unafanya nini mahali hapa? Kwa nini uko hapa?”
4
Akawaeleza yale Mika aliyomtendea, naye akasema, “Ameniajiri nami ni kuhani wake.”
5
Kisha wakamwambia, “Tafadhali tuulizie kwa Mungu kama safari yetu itafanikiwa.”
6
Yule kuhani akawajibu, “Enendeni kwa amani. Safari yenu ina kibali cha Bwana.”
7
Basi hao watu watano wakaondoka na kufika Laishi, mahali ambapo waliwakuta watu wanaishi salama, kama Wasidoni, kwa utulivu na bila mashaka. Nchi yao haikupungukiwa na kitu chochote, hivyo wakawa tajiri. Pia walikaa mbali sana na Wasidoni, wala hawakushughulika na mtu yeyote.
8
Waliporudi kwa ndugu zao huko Sora na Eshtaoli, ndugu zao wakawauliza, “Mlionaje mambo huko?”
9
Wakajibu, “Twendeni, tukapigane nao! Tumeona kuwa nchi ni nzuri sana. Je, hamtafanya chochote? Msisite kupanda ili kuimiliki.
10
Mtakapokwenda huko mtakuta watu waliotulia walio salama, nayo nchi hiyo ni kubwa na Mungu ameitia mikononi mwenu, nayo ni nchi ambayo haikupungukiwa na kitu chochote kilicho duniani.”
11
Ndipo watu 600 toka ukoo wa Wadani, waliojifunga silaha za vita, wakaondoka Sora na Eshtaoli.
12
Walipokuwa wakisafiri wakapiga kambi huko Kiriath-Yearimu katika Yuda. Hii ndiyo sababu sehemu ya magharibi ya Kiriath-Yearimu inaitwa Mahane-Dani mpaka leo.
13
Kutoka hapo wakaendelea mbele mpaka nchi ya vilima ya Efraimu na kufika katika nyumba ya Mika.
14
Ndipo wale watu watano waliopeleleza nchi ya Laishi wakawaambia ndugu zao, “Je, mwajua kuwa mojawapo ya nyumba hizi kuna naivera, sanamu ndogo za nyumbani, sanamu ya kuchonga na sanamu ya kusubu? Sasa basi fikirini mtakalofanya.”
15
Basi wakaingia humo na kwenda kwenye nyumba ya yule kijana Mlawi katika nyumba ya Mika na kumsalimu.
16
Wale Wadani 600, waliovaa silaha za vita, wakasimama penye ingilio la lango.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings