Mwanzo 42:25-35
25
Yosefu akatoa amri ya kujaza magunia yao nafaka na kuweka fedha ya kila mmoja ndani ya gunia lake, kisha wapewe mahitaji ya njiani. Baada ya kufanyiwa hayo yote,
26
wakapakiza nafaka juu ya punda zao, wakaondoka.
27
Walipofika mahali pa kulala huko njiani mmoja wao akafungua gunia lake ili amlishe punda wake, akakuta fedha yake kwenye mdomo wa gunia lake.
28
Akawaambia ndugu zake, “Fedha yangu imerudishwa. Iko ndani ya gunia langu.” Mioyo yao ikazimia, na kila mmoja akamgeukia mwenzake wakitetemeka, wakaulizana, “Ni nini hiki Mungu alichotufanyia?”
29
Walipofika kwa Yakobo baba yao katika nchi ya Kanaani, wakamweleza mambo yote yaliyowapata. Wakasema,
30
“Huyo mtu ambaye ndiye bwana katika nchi hiyo alisema nasi kwa ukali, akatutendea kana kwamba sisi tulikuwa tunaipeleleza nchi.
31
Lakini tulimwambia, ‘Sisi ni watu waaminifu, sio wapelelezi.
32
Tulizaliwa ndugu kumi na wawili, wana wa baba mmoja. Mmoja alikufa, na mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu huko Kanaani.’
33
“Ndipo huyo mtu aliye bwana katika nchi hiyo alipotuambia, ‘Hivi ndivyo nitafahamu kuwa ninyi ni watu waaminifu: Mwacheni mmoja wa ndugu zenu pamoja nami hapa, kisha nendeni mpeleke chakula kwa ajili ya jamaa yenu inayoteseka kwa njaa.
34
Lakini mleteni huyo ndugu yenu mdogo kwangu, ndipo nitajua kuwa ninyi sio wapelelezi, ila ni watu waaminifu. Kisha nitamrudisha ndugu yenu, nanyi mtaweza kufanya biashara katika nchi hii.’ ”
35
Walipokuwa wanamimina nafaka kutoka kwenye magunia yao, ndani ya gunia la kila mtu kulikuwa na mfuko wa fedha! Wakati wao na baba yao walipoona mifuko ya fedha, wakaogopa.
Settings