Mwanzo 42:6-17
6
Wakati huo Yosefu alikuwa mtawala wa nchi ya Misri, naye alikuwa ndiye aliwauzia watu wote nafaka. Kwa hiyo wakati ndugu zake Yosefu walipofika, wakamsujudia hadi nyuso zao zikagusa ardhi.
7
Mara Yosefu alipowaona ndugu zake, akawatambua, lakini akajifanya mgeni na kuzungumza nao kwa ukali, akiwauliza, “Ninyi mnatoka wapi?” Wakamjibu, “Tumetoka katika nchi ya Kanaani kuja kununua chakula.”
8
Ingawa Yosefu aliwatambua ndugu zake, wao hawakumtambua.
9
Ndipo Yosefu alipokumbuka ndoto zake kuwahusu wao, akawaambia, “Ninyi ni wapelelezi! Mmekuja kuangalia mahali ambapo nchi yetu haina ulinzi.”
10
Wakamjibu, “Sivyo bwana wangu. Watumishi wako wamekuja kununua chakula.
11
Sisi sote ni wana wa baba mmoja. Watumishi wako ni watu waaminifu, wala sio wapelelezi.”
12
Akawaambia, “La hasha! Mmekuja kuangalia mahali ambapo nchi yetu haina ulinzi.”
13
Lakini wakamjibu, “Watumishi wako walikuwa kumi na wawili, wana wa mtu mmoja ambaye anaishi katika nchi ya Kanaani. Sasa mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu na mwingine alikufa.”
14
Yosefu akawaambia, “Ni sawa kabisa kama nilivyowaambia: Ninyi ni wapelelezi!
15
Na hivi ndivyo mtakavyojaribiwa: Hakika kama Farao aishivyo, hamtaondoka mahali hapa mpaka ndugu yenu mdogo aje hapa.
16
Tumeni mmoja wenu akamlete huyo ndugu yenu, wengine mtawekwa gerezani, ili maneno yenu yajaribiwe kuona kama mnasema kweli. La sivyo, hakika kama Farao aishivyo ninyi ni wapelelezi!”
17
Akawaweka wote chini ya ulinzi kwa siku tatu.
Settings