Mwanzo 14:13-24
13
Mtu mmoja aliyekuwa ametoroka akaja kumpa Abramu Mwebrania taarifa. Wakati huu Abramu alikuwa anaishi karibu na mialoni ya Mamre Mwamori, aliyekuwa ndugu yake Eshkoli na Aneri, ambao wote walikuwa wameungana na Abramu.
14
Abramu alipopata habari kwamba jamaa yake amechukuliwa mateka, akawaita watu 318 wa nyumbani mwake waliokuwa wamefunzwa kupigana vita, wakawafuatilia hadi Dani.
15
Wakati wa usiku Abramu aliwagawa watu wake katika vikosi ili awashambulie, na akawafuatilia, akawafukuza hadi Hoba, kaskazini ya Dameski.
16
Akarudisha mali zote, na akamrudisha Loti jamaa yake na mali zake, pamoja na wanawake na watu wengine.
17
Abramu aliporudi baada ya kumshinda Mfalme Kedorlaoma na wale wafalme waliojiunga naye, mfalme wa Sodoma akatoka kwenda kumlaki katika Bonde la Shawe (yaani Bonde la Mfalme).
18
Ndipo Melkizedeki mfalme wa Salemu alipoleta mkate na divai. Alikuwa kuhani wa Mungu Aliye Juu Sana.
19
Naye akambariki Abramu, akisema, “Abarikiwe Abramu na Mungu Aliye Juu Sana, Muumba wa mbingu na nchi.
20
Abarikiwe Mungu Aliye Juu Sana, ambaye amewaweka adui zako mkononi mwako.” Ndipo Abramu akampa Melkizedeki sehemu ya kumi ya kila kitu.
21
Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, “Nipe hao watu na hizo mali uchukue wewe mwenyewe.”
22
Lakini Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, “Nimeinua mkono wangu kwa Bwana, Mungu Aliye Juu Sana, Muumba wa mbingu na dunia, na nimeapa
23
kwamba sitapokea kitu chochote kilicho chako, hata kama ni uzi au gidamu ya kiatu, ili kamwe usije ukasema, ‘Nimemtajirisha Abramu.’
24
Sitapokea chochote, ila kile tu watu wangu walichokula na sehemu ambayo ni fungu la watu waliokwenda pamoja nami, ambao ni Aneri, Eshkoli na Mamre. Wao na wapewe fungu lao.”
Settings