Skip to content
Ezekieli 3:9-27

Ezekieli 3:9-27

9
Kama vile almasi ilivyo ngumu kuliko gumegume, ndivyo nilivyokifanya kipaji cha uso wako. Usiwaogope wala usiwahofu, ijapokuwa ni nyumba ya kuasi.”
10
Naye akaniambia, “Mwanadamu, sikiliza kwa makini na uyatie moyoni mwako maneno yote nitakayosema nawe.
11
Kisha nenda kwa watu wa taifa lako walio uhamishoni, ukaseme nao. Waambie, ‘Hivi ndivyo Bwana Mwenyezi asemavyo,’ kwamba watasikiliza au hawatasikiliza.”
12
Ndipo Roho akaniinua, nikasikia sauti kubwa nyuma yangu ya ngurumo. (Utukufu wa Bwana na utukuzwe katika mahali pa makao yake!)
13
Ilikuwa ni sauti ya mabawa ya wale viumbe hai yakisuguana moja kwa jingine, sauti kama ya ngurumo.
14
Ndipo Roho aliponiinua na kunipeleka mbali. Nikaenda nikiwa na uchungu na hasira moyoni mwangu, nao mkono wa Bwana ukiwa juu yangu.
15
Nikafika kwa wale watu waliokuwa uhamishoni huko Tel-Abibu karibu na Mto Kebari. Nikakaa miongoni mwao kwa muda wa siku saba, nikiwa nimejawa na mshangao.
16
Mwishoni mwa hizo siku saba neno la Bwana likanijia kusema:
17
“Mwanadamu, nimekufanya uwe mlinzi wa nyumba ya Israeli, kwa hiyo sikia neno nisemalo, ukawape onyo litokalo kwangu.
18
Nimwambiapo mtu mwovu, ‘Hakika utakufa,’ na wewe usipomwonya mtu huyo au kumshauri aache njia zake mbaya ili kuokoa maisha yake, huyo mtu mwovu atakufa katika dhambi yake na damu yake nitaidai mkononi mwako.
19
Lakini ukimwonya mtu mwovu naye akakataa kuacha uovu wake na njia zake mbaya, atakufa katika dhambi yake, lakini wewe utakuwa umejiokoa nafsi yako.
20
“Tena, mtu mwenye haki akiacha haki yake na kutenda maovu, nami nikaweka kikwazo mbele yake mtu huyo atakufa. Kwa kuwa hukumwonya, atakufa katika dhambi yake. Mambo ya haki aliyotenda, hayatakumbukwa, damu yake nitaidai mkononi mwako.
21
Lakini ukimwonya mwenye haki asitende dhambi na akaacha kutenda dhambi, hakika ataishi kwa sababu alipokea maonyo na utakuwa umejiokoa nafsi yako.”
22
Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu huko, naye akaniambia, “Simama uende mpaka sehemu tambarare, nami nitasema nawe huko.”
23
Kwa hiyo niliinuka nikaenda mpaka mahali pa tambarare. Utukufu wa Bwana ulikuwa umesimama huko, kama utukufu ule niliouona kando ya Mto Kebari, nami nikaanguka kifudifudi.
24
Ndipo Roho akaja ndani yangu akanisimamisha kwa miguu yangu. Akasema nami akaniambia: “Nenda ukajifungie ndani ya nyumba yako.
25
Nawe, ee mwanadamu, watakufunga kwa kamba, watakufunga ili usiweze kutoka na kuwaendea watu.
26
Nitaufanya ulimi wako ushikamane kwenye kaa la kinywa chako, ili uwe kimya usiweze kuwakemea, wajapokuwa ni nyumba ya kuasi.
27
Lakini nitakaposema nawe, nitafungua kinywa chako nawe utawaambia, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo.’ Yeyote atakayesikiliza na asikilize, na yeyote atakayekataa na akatae; kwa kuwa wao ni nyumba ya kuasi.

Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.

Settings

Reading style

Typeface

Font size 19px

Reading width 75 chars

Options