Skip to content
Kutoka 14:1-18

Kutoka 14:1-18

1
Ndipo Bwana akamwambia Mose,
2
“Waambie Waisraeli wageuke nyuma na wapige kambi karibu na Pi-Hahirothi, kati ya Migdoli na bahari. Watapiga kambi kando ya bahari, mkabala na Baal-Sefoni.
3
Farao atafikiri kwamba, ‘Hao Waisraeli wanatangatanga katika nchi kwa kuchanganyikiwa, nalo jangwa limewafungia.’
4
Nami nitaufanya moyo wa Farao mgumu, naye atawafuatilia. Lakini nitajipatia utukufu kwa ajili yangu mwenyewe kupitia Farao na jeshi lake lote, nao Wamisri watajua kuwa mimi ndimi Bwana.” Kwa hiyo Waisraeli wakafanya hivyo.
5
Mfalme wa Misri alipoambiwa kuwa Waisraeli wamekimbia, Farao na maafisa wake wakabadili nia zao kuhusu Waisraeli, wakasema, “Tumefanya nini? Tumewaachia Waisraeli waende zao na tumeukosa utumishi wao!”
6
Kwa hiyo akaandaliwa gari lake la vita, naye akaenda pamoja na jeshi lake.
7
Akachukua magari bora mia sita, pamoja na magari mengine yote ya Misri, pamoja na maafisa wa magari hayo yote.
8
Bwana akaufanya mgumu moyo wa Farao, mfalme wa Misri, kwa hiyo akawafuatia Waisraeli, waliokuwa wakiondoka Misri kwa ujasiri.
9
Nao Wamisri, yaani farasi wote wa Farao na magari ya vita, wapanda farasi na vikosi vya askari, wakawafuatia Waisraeli, wakawakuta karibu na Pi-Hahirothi, mkabala na Baal-Sefoni walipokuwa wamepiga kambi kando ya bahari.
10
Farao alipokaribia, Waisraeli wakainua macho yao, wakawaona Wamisri wakija nyuma yao. Wakashikwa na hofu, wakamlilia Bwana.
11
Wakamwambia Mose, “Je, ni kwamba hayakuwako makaburi huko Misri hata umetuleta tufe huku jangwani? Umetufanyia nini kututoa Misri?
12
Hatukukuambia tulipokuwa huko Misri, tuache tuwatumikie Wamisri? Ingekuwa vyema zaidi kwetu kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani!”
13
Mose akawajibu Waisraeli, “Msiogope. Simameni imara, nanyi mtauona wokovu Bwana atakaowapatia leo. Hao Wamisri mnaowaona leo kamwe hamtawaona tena.
14
Bwana atawapigania ninyi, nanyi mnatakiwa kutulia tu.”
15
Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Kwa nini wewe unanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele.
16
Inua fimbo yako na unyooshe mkono wako juu ya bahari ili kuyagawa maji, hivyo kwamba Waisraeli wapate kupita mahali pakavu baharini.
17
Nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu kusudi waingie baharini wakiwafuatia. Nami nitajipatia utukufu kupitia Farao pamoja na jeshi lake lote, kupitia magari yake ya vita na wapanda farasi wake.
18
Nao Wamisri watajua kwamba Mimi ndimi Bwana nitakapojipatia utukufu kupitia Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake.”

Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.

Settings

Reading style

Typeface

Font size 19px

Reading width 75 chars

Options