Skip to content

Mistari ya Biblia kuhusu Vashti

17 mistari · 1 kipengele

Mistari muhimu ya Biblia

  1. Malkia Vashti pia akawafanyia wanawake karamu katika jumba la kifalme la Mfalme Ahasuero.

  2. Siku ya saba, wakati Mfalme Ahasuero alikuwa amesisimka roho yake kwa mvinyo, aliamuru matowashi saba waliokuwa wakimhudumia, yaani, Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari na Karkasi,

  3. kumleta Malkia Vashti mbele ya mfalme akiwa amevaa taji lake la kifalme, ili aonyeshe uzuri wake kwa watu na wakuu, kwa kuwa alikuwa ni mzuri wa kupendeza.

  4. Lakini wakati watumishi walipotoa amri ya mfalme, Malkia Vashti alikataa kuja. Ndipo mfalme alighadhibika, na hasira yake ikawaka.

  5. Kwa kuwa ilikuwa desturi ya mfalme kupata ushauri kwa wataalamu katika mambo ya sheria na haki, alizungumza na watu wenye busara, ambao walijua nyakati,

  6. nao waliokuwa karibu na mfalme ni Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena na Memukani, wakuu saba wa Uajemi na Umedi waliokuwa na nafasi ya pekee kwa mfalme nao walikuwa na vyeo vya juu kabisa katika utawala wake.

  7. Mfalme akauliza, “Kulingana na sheria, Malkia Vashti anapaswa kutendewa nini? Malkia hakutii amri ya Mfalme Ahasuero ambayo matowashi walimpelekea.”

  8. Kisha Memukani akajibu mbele ya mfalme na wakuu, “Malkia Vashti si kwamba amemkosea mfalme tu bali pia amewakosea wakuu wote na watu wa himaya yote ya Mfalme Ahasuero.

  9. Kwa maana tendo hili la malkia litajulikana kwa wanawake wote, kwa hiyo watawadharau waume zao na kusema, ‘Mfalme Ahasuero aliagiza Malkia Vashti aletwe mbele yake, lakini alikataa.’

  10. Leo hii wanawake wa wakuu wa Uajemi na Umedi ambao wamesikia juu ya tabia ya malkia watawatendea wakuu wote wa mfalme vivyo hivyo. Hapatakuwepo na mwisho wa dharau na magomvi.

  11. “Kwa hiyo, kama itampendeza mfalme, atoe amri ya kifalme na iandikwe katika sheria ya Uajemi na Umedi, ambayo haitabadilika, kwamba Vashti kamwe asije tena mbele ya Mfalme Ahasuero. Pia mfalme na atoe hiyo nafasi yake ya umalkia kwa mwanamke mwingine aliye bora kumliko yeye.

  12. Kisha mbiu hii ya mfalme itakapotangazwa katika himaya yake iliyo kubwa sana, wanawake wote watawaheshimu waume zao, kuanzia mdogo hadi mkubwa.”

  13. Mfalme na wakuu wake walipendezwa na shauri hili, hivyo basi mfalme akafanya kama Memukani alivyopendekeza.

  14. Alipeleka barua katika sehemu zote za ufalme wake, kwa kila jimbo kwa maandishi yake mwenyewe na kwa kila watu katika lugha yao wenyewe, akitangaza kwa msemo wa kila watu kwamba inampasa kila mwanaume kuwa mtawala wa nyumba yake mwenyewe.

  15. Baadaye, wakati hasira ya Mfalme Ahasuero ilikuwa imetulia, alimkumbuka Vashti na kile alichokuwa amekifanya na alilokuwa ameamuru juu yake.

  16. Kisha yule ambaye atampendeza mfalme na awe malkia badala ya Vashti.” Shauri hili likampendeza mfalme, naye akalifuata.

  17. Basi ikawa mfalme alivutiwa na Esta kuliko wanawake wengine wote, naye akapata upendeleo na kibali kuliko mabikira wengine. Kisha akamvika taji la kifalme kichwani mwake na kumfanya malkia badala ya Vashti.