Mathayo 26:59-75
59
Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu ili wapate kumuua.
60
Lakini hawakupata jambo lolote, ingawa mashahidi wengi wa uongo walijitokeza. Hatimaye wakajitokeza mashahidi wawili wa uongo
61
na kusema, “Huyu mtu alisema, ‘Ninaweza kulivunja Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’ ”
62
Kisha kuhani mkuu akasimama na kumwambia Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?”
63
Lakini Yesu akakaa kimya. Ndipo kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha mbele za Mungu aliye hai. Tuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu.”
64
Yesu akajibu, “Wewe umenena. Lakini ninawaambia nyote: Siku za baadaye, mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”
65
Ndipo kuhani mkuu akararua mavazi yake na kusema, “Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? Tazama, sasa ninyi mmesikia hayo makufuru.
66
Uamuzi wenu ni gani?” Wakajibu, “Anastahili kufa.”
67
Kisha wakamtemea mate usoni na wengine wakampiga ngumi. Wengine wakampiga makofi
68
na kusema, “Tutabirie, wewe Kristo! Ni nani aliyekupiga?”
69
Wakati huu Petro alikuwa amekaa nje uani. Mtumishi mmoja wa kike akamjia na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.”
70
Lakini Petro akakana mbele yao wote akisema, “Sijui hilo usemalo.”
71
Alipotoka nje kufika kwenye lango, mtumishi mwingine wa kike alimwona, akawaambia watu waliokuwepo, “Huyu mtu alikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.”
72
Akakana tena kwa kiapo akisema, “Mimi simjui huyo!”
73
Baada ya muda mfupi, wale waliokuwa wamesimama pale wakamwendea Petro, wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana usemi wako ni kama wao.”
74
Ndipo Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui mtu huyo!” Papo hapo jogoo akawika.
75
Ndipo Petro akakumbuka lile neno Yesu alilokuwa amesema: “Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Naye akaenda nje, akalia kwa majonzi.
Settings