Skip to content
Waamuzi 19:11-30

Waamuzi 19:11-30

11
Alipokaribia Yebusi na usiku ukiwa umekaribia, mtumishi akamwambia bwana wake, “Haya sasa natuingie katika mji huu wa Wayebusi tulale humo.”
12
Lakini bwana wake akamjibu, “Hapana. Hatutaingia kwenye mji wa kigeni, ambao watu wake si Waisraeli. Tutaendelea mpaka tufike Gibea.”
13
Akasema, “Haya, tujitahidi tufike Gibea au Rama, nasi tutalala katika mji mmojawapo.”
14
Hivyo wakaendelea na safari, jua likachwea walipokaribia Gibea ambao ni mji wa Benyamini.
15
Wakageuka ili kuingia na kulala Gibea. Wakaingia humo, wakaketi kwenye uwanja wa mji, wala hakuna mtu yeyote aliyewakaribisha kwake ili wapate kulala.
16
Jioni ile mtu mmoja mzee toka nchi ya vilima ya Efraimu, aliyekuwa anaishi huko Gibea (watu wa sehemu ile walikuwa Wabenyamini), akarudi kutoka kwenye kazi za shamba.
17
Alipotazama na kuwaona hao wasafiri katika uwanja wa mji, yule mzee akawauliza, “Ninyi mnakwenda wapi? Nanyi mmetoka wapi?”
18
Akamwambia, “Tumepita kutoka Bethlehemu ya Yuda, tunaelekea katika nchi ya vilima ya Efraimu, ambako ndiko ninakoishi. Nilikwenda Bethlehemu ya Yuda na sasa ninakwenda katika nyumba ya Bwana. Hakuna mtu yeyote aliyenikaribisha katika nyumba yake.
19
Tunazo nyasi na chakula cha punda wetu na mkate na divai kwa ajili yetu sisi watumishi wako, yaani mimi, mtumishi wako mwanamke, pamoja na huyu kijana tuliyefuatana naye. Hatuhitaji kitu chochote.”
20
Yule mzee akawaambia, “Amani iwe kwenu! Karibuni nyumbani mwangu. Nitawapa mahitaji yenu yote, msilale katika uwanja huu wa mji.”
21
Hivyo akamwingiza nyumbani mwake na kuwalisha punda wake. Baada ya kunawa miguu yao, wakala na kunywa.
22
Walipokuwa wakijiburudisha, watu waovu wa mji huo, wakaizingira ile nyumba. Wakagonga mlango na kusema na yule mzee mwenye nyumba, “Mtoe nje yule mtu aliyeingia kwako, tupate kumlawiti.”
23
Yule mwenye nyumba akatoka nje na kuwaambia, “Hapana, ndugu zangu msiwe waovu namna hii, ninawasihi. Kwa kuwa huyu mtu ni mgeni wangu msifanye jambo hili la aibu.
24
Tazameni, hapa yupo binti yangu ambaye ni bikira na suria wa huyu mtu. Nitawatoleeni hawa sasa, mkawatwae kwa nguvu na kuwafanyia lolote mtakalo. Lakini kwa mtu huyu msimfanyie jambo ovu hivyo.”
25
Lakini wale watu hawakumsikia. Hivyo yule mtu akamtoa yule suria wake nje kwa wale watu, nao wakambaka na kumnajisi usiku ule kucha mpaka asubuhi. Kulipoanza kupambazuka wakamwachia aende.
26
Alfajiri yule mwanamke akarudi kwenye ile nyumba bwana wake alikokuwa, akaanguka chini mlangoni, akalala pale hata kulipopambazuka.
27
Bwana wake alipoamka asubuhi na kufungua mlango wa nyumba na kutoka nje ili kuendelea na safari yake, tazama, yule suria wake alikuwa ameanguka pale penye ingilio la nyumba na mikono yake ikiwa penye kizingiti cha chini.
28
Akamwambia yule suria, “Inuka, twende.” Lakini hakujibu. Yule bwana akamwinua akampandisha juu ya punda wake, wakaondoka kwenda nyumbani.
29
Alipofika nyumbani, akachukua kisu na kumkatakata yule suria kiungo kwa kiungo, sehemu kumi na mbili, na kuvipeleka hivyo vipande katika sehemu zote za Israeli.
30
Kila mtu aliyeona akasema, “Jambo la namna hii halijaonekana wala kutendeka, tangu Israeli walipopanda kutoka Misri. Fikirini juu ya jambo hili! Tafakarini juu ya jambo hili! Tuambieni tufanye nini!”

Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.

Settings

Reading style

Typeface

Font size 19px

Reading width 75 chars

Options