Skip to content
Yoshua 22:21-34

Yoshua 22:21-34

21
Ndipo Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase walipowajibu viongozi wa koo za Israeli, wakisema:
22
“Yeye Mwenye Nguvu, Mungu, Bwana! Yeye Mwenye Nguvu, Mungu, Bwana! Yeye anajua! Israeli na wajue! Kama huu umekuwa ni uasi au kukosa utii kwa Bwana, msituache hai siku hii ya leo.
23
Kama tumejijengea madhabahu yetu wenyewe ili kumwacha Bwana na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka, au kutoa sadaka za amani juu yake, Bwana mwenyewe na atupatilize leo.
24
“Sivyo! Tulifanya hivyo kwa hofu kwamba siku zijazo wazao wenu wanaweza wakawaambia wazao wetu, ‘Mna uhusiano gani na Bwana, Mungu wa Israeli?
25
Bwana ameifanya Yordani kuwa mpaka kati yetu na ninyi, ninyi Wareubeni na Wagadi! Hamna fungu kwa Bwana.’ Kwa hiyo wazao wenu wanaweza wakawasababisha wazao wetu wakaacha kumcha Bwana.
26
“Hii ndiyo sababu tulisema, ‘Tujiweke tayari na tujenge madhabahu, lakini si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa au dhabihu.’
27
Badala yake, itakuwa ni ushahidi kati yetu na ninyi na vizazi vijavyo, kwamba tutamwabudu Bwana katika mahali patakatifu pake pamoja na sadaka zetu za kuteketezwa, dhabihu na sadaka za amani. Ndipo katika siku zijazo, wazao wenu hawataweza kuwaambia wazao wetu, ‘Ninyi hamna fungu katika Bwana.’
28
“Nasi tulisema, ‘Ikiwa wakati wowote watatuambia hilo, au kuwaambia uzao wetu, tutawajibu hivi: Angalieni nakala hii ya madhabahu ya Bwana, ambayo baba zetu waliijenga, si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa na dhabihu, bali kama ushahidi kati yetu na ninyi.’
29
“Hili jambo la kumwasi Bwana na kumwacha siku hii ya leo kwa kujenga madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na dhabihu, zaidi ya madhabahu ya Bwana Mungu wetu iliyo mbele ya maskani yake na liwe mbali nasi.”
30
Wakati kuhani Finehasi na viongozi wa kusanyiko na wakuu wa koo za Israeli, waliposikia hayo waliyosema Wareubeni, Wagadi na Manase, wakaridhika.
31
Naye Finehasi mwana wa kuhani Eleazari, akawaambia Wareubeni, Wagadi na Manase, “Leo tunajua kwamba Bwana yuko pamoja nasi, kwa sababu hamkukosa uaminifu kwa Bwana katika jambo hili. Sasa mmewaokoa Waisraeli na mkono wa Bwana.”
32
Ndipo Finehasi, mwana wa kuhani Eleazari na viongozi wakarudi Kanaani kutoka kwenye kukutana kwao na Wareubeni na Wagadi huko Gileadi nao wakatoa taarifa kwa Waisraeli.
33
Walifurahi kusikia taarifa hiyo, na wakamhimidi Mungu. Wala hawakuzungumza tena habari za kupigana vita dhidi yao ili kuharibu nchi ambayo Wareubeni na Wagadi waliishi.
34
Nao Wareubeni na Wagadi wakayaita yale madhabahu Edi, yaani Shahidi: kwa kuwa itakuwa shahidi kati yetu na ninyi kwamba Bwana ndiye Mungu.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options