Kutoka 12:17-41
17
“Mtaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, kwa sababu hiyo ndiyo siku ile niliyovitoa vikosi vyenu kutoka Misri. Mtaiadhimisha siku hii kwa vizazi vyenu vyote kuwa amri ya kudumu.
18
Katika mwezi wa kwanza mtakula mikate isiyotiwa chachu, kuanzia jioni ya siku ya kumi na nne hadi jioni ya siku ya ishirini na moja.
19
Kwa muda wa siku saba isionekane chachu yoyote katika nyumba zenu. Yeyote alaye chochote chenye chachu ndani yake, lazima akatiliwe mbali kutoka jumuiya ya Israeli, akiwa ni mgeni au mzawa.
20
Msile chochote kilichotiwa chachu. Popote muishipo, ni lazima mle mikate isiyotiwa chachu.”
21
Ndipo Mose akawaita wazee wote wa Israeli na kuwaambia, “Nendeni mara moja mkachague wanyama kwa ajili ya jamaa zenu, mkachinje mwana-kondoo wa Pasaka.
22
Chukueni kitawi cha hisopo, kichovyeni kwenye damu iliyopo kwenye sinia na kuipaka baadhi ya hiyo damu kwenye vizingiti na kwenye miimo yote miwili ya milango. Mtu yeyote asitoke nje ya mlango wa nyumba yake mpaka asubuhi.
23
Bwana apitapo katika nchi yote kuwapiga Wamisri, ataiona damu juu ya vizingiti na kwenye miimo ya milango, naye atapita juu, wala hatamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwapiga ninyi.
24
“Shikeni maagizo haya yawe kanuni ya kudumu kwenu na kwa ajili ya wazao wenu.
25
Mtakapoingia katika nchi Bwana atakayowapa kama alivyoahidi, shikeni desturi hii.
26
Watoto wenu watakapowauliza, ‘Sikukuu hii ina maana gani kwenu?’
27
Basi waambieni, ‘Hii ni dhabihu ya Pasaka kwa Bwana, ambaye alipita juu ya nyumba za Waisraeli katika nchi ya Misri na hakudhuru nyumba zetu alipowapiga Wamisri.’ ” Ndipo watu wa Israeli waliposujudu na kuabudu.
28
Waisraeli wakafanya kama vile Bwana alivyomwagiza Mose na Aroni.
29
Ilipofika usiku wa manane, Bwana akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika Misri, kuanzia mzaliwa wa kwanza wa Farao, mrithi wa kiti cha ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa mfungwa, aliyekuwa gerezani, na wazaliwa wa kwanza wa mifugo yote pia.
30
Farao, na maafisa wake wote, na Wamisri wote wakaamka usiku, na kulikuwa na kilio kikubwa katika nchi ya Misri, kwa kuwa haikuwepo nyumba ambayo hakufa mtu.
31
Wakati huo Farao akawaita Mose na Aroni na kuwaambia, “Ondokeni! Tokeni kwa watu wangu, ninyi pamoja na Waisraeli! Nendeni mkamwabudu Bwana kama mlivyoomba.
32
Chukueni makundi yenu ya kondoo na mbuzi pamoja na ngʼombe, kama mlivyosema, nanyi mwende zenu. Nanyi pia mnibariki.”
33
Wamisri wakawahimiza Waisraeli waondoke kwa haraka na kuacha nchi yao. Kwa kuwa walisema, “La sivyo, tutakufa wote!”
34
Hivyo watu wakachukua donge lao la unga kabla ya kutiwa chachu, wakaweka ndani ya mabakuli ya kukandia, wakayaviringisha katika vitambaa na kuyabeba mabegani mwao.
35
Waisraeli wakafanya kama Mose alivyowaelekeza, nao wakawaomba Wamisri wawapatie vitu vya fedha, dhahabu na nguo.
36
Basi Bwana alikuwa amewafanya Wamisri kuwa wakarimu kwa hawa watu, wakawapatia Waisraeli vile walivyotaka kwao; kwa hiyo wakawateka nyara Wamisri.
37
Waisraeli wakasafiri kutoka Ramesesi mpaka Sukothi. Walikuwepo wanaume wapatao 600,000 waendao kwa miguu bila kuhesabu wanawake na watoto.
38
Watu wengine wengi wakafuatana nao, pamoja na makundi makubwa ya mifugo wakiwemo kondoo, mbuzi na ngʼombe.
39
Wakatengeneza maandazi yasiyotiwa chachu kwa ule unga uliokandwa waliokuwa wameutoa Misri, donge hilo la unga halikuwa limetiwa chachu, kwa kuwa walikuwa wameondolewa Misri kwa haraka nao hawakuwa na muda wa kuandaa chakula chao.
40
Waisraeli walikuwa wameishi Misri kwa muda wa miaka 430.
41
Ilikuwa ni siku ya mwisho ya hiyo miaka 430, vikosi vyote vya Bwana vilipokuwa vimeondoka Misri.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings