1 Wafalme 22:22-38
22
“Bwana akauliza, ‘Kwa njia gani?’ “Akasema, ‘Nitakwenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote.’ “Bwana akasema, ‘Utafanikiwa katika kumshawishi. Nenda ukafanye hivyo.’
23
“Kwa hiyo sasa Bwana ameweka roho ya kudanganya ndani ya vinywa vya hawa manabii wako wote. Bwana ameamuru maafa kwa ajili yako.”
24
Kisha Sedekia mwana wa Kenaana akatoka na kumpiga Mikaya kofi usoni. Akauliza, “Huyo Roho kutoka kwa Bwana alipita njia gani alipotoka kwangu ili kusema nawe?”
25
Mikaya akajibu, “Utagundua siku hiyo utakapokwenda kujificha kwenye chumba cha ndani.”
26
Kisha mfalme wa Israeli akaagiza, “Mchukueni na mkamrudishe kwa Amoni mtawala wa mji na kwa Yoashi mwana wa mfalme.
27
Mkaseme, ‘Hivi ndivyo asemavyo mfalme: Mwekeni mtu huyu gerezani na asipewe chochote ila mkate na maji mpaka nitakaporudi salama.’ ”
28
Mikaya akasema, “Kama utarudi salama, basi Bwana hajanena kupitia kwangu.” Kisha akaongeza kusema, “Zingatieni maneno yangu, enyi watu wote!”
29
Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakaenda Ramoth-Gileadi.
30
Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Nitaingia vitani nikiwa nimejibadilisha, lakini wewe uvae majoho yako ya kifalme.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akajibadilisha na kwenda vitani.
31
Wakati huu, mfalme wa Aramu alikuwa amewaagiza majemadari thelathini na wawili wa magari ya vita, “Msipigane na yeyote, mdogo au mkubwa, isipokuwa mfalme wa Israeli.”
32
Wakati wale majemadari wa magari ya vita walipomwona Yehoshafati wakafikiri, “Hakika huyu ndiye mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo wakageuka ili wamshambulie, lakini Yehoshafati akapiga kelele,
33
wale majemadari wakaona kwamba hakuwa mfalme wa Israeli, nao wakaacha kumfuatilia.
34
Lakini mtu fulani akavuta upinde pasipo lengo na kumpiga mfalme wa Israeli katikati ya kiungio cha mavazi yake ya chuma. Mfalme akamwambia mwendesha gari lake, “Geuza gari na uniondoe mimi katika mapigano, nimejeruhiwa.”
35
Vita vikaendelea mchana kutwa, naye Mfalme Ahabu akategemezwa ndani ya gari kuelekea Waaramu. Damu kutoka kwenye jeraha lake ikachuruzika ndani ya gari na jioni yake akafa.
36
Jua lilipokuwa linazama, mbiu ikaenea katika jeshi lote: “Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake!”
37
Basi mfalme akafa na akaletwa Samaria, nao wakamzika huko.
38
Wakasafisha lile gari la vita katika bwawa la Samaria (mahali makahaba walipooga), na mbwa wakaramba damu yake, sawasawa na neno la Bwana lilivyokuwa limesema.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings