Rukia maudhui

Zekaria11

Unabii wa Uharibifu na Hukumu

1
Fungua milango yako, ee Lebanoni, ili moto uteketeze mierezi yako!
2
Piga yowe, ee mti wa msunobari, kwa kuwa mwerezi umeanguka; miti ya fahari imeharibiwa! Piga yowe, enyi mialoni ya Bashani, msitu mnene umefyekwa!
3
Sikiliza yowe la wachungaji; malisho yao manono yameangamizwa! Sikia ngurumo za simba; kichaka kilichostawi sana cha Yordani kimeharibiwa!

Agizo la Kulilisha Kundi Lililohukumiwa

4
Hili ndilo asemalo Bwana Mungu wangu: “Lilishe kundi lililokusudiwa kuchinjwa.
5
Wanunuzi wake huwachinja na kuondoka pasipo kuadhibiwa. Wale wanaowauza husema, ‘Bwana asifiwe, mimi ni tajiri!’ Wachungaji wao wenyewe hawawahurumii.
6
Kwa kuwa sitawahurumia tena watu wa nchi,” asema Bwana. “Nitawakabidhi kila mtu mkononi mwa jirani yake na mfalme wake. Wataitenda jeuri nchi, nami sitawaokoa kutoka mikononi mwao.”

Matendo ya Kiishara ya Mchungaji wa Kweli

7
Kwa hiyo nikalilisha kundi lililotiwa alama kwa kuchinjwa, hasa kundi lililoonewa sana. Kisha nikachukua fimbo mbili, moja nikaiita Fadhili na nyingine Umoja, nami nikalilisha kundi.
8
Katika mwezi mmoja nikawaondoa wachungaji watatu. Kundi la kondoo likanichukia, nami nikachoshwa nao,
9
nikasema, “Sitakuwa mchungaji wenu. Waache wanaokufa wafe na wanaoangamia waangamie. Wale waliobakia kila mmoja na ale nyama ya mwenzake.”
10
Kisha nikachukua fimbo yangu inayoitwa Fadhili nikaivunja, kutangua Agano nililofanya na mataifa yote.
11
Likatanguka siku hiyo, kwa hiyo wale waliodhurika katika kundi, waliokuwa wakiniangalia wakajua kuwa hilo lilikuwa neno la Bwana.
12
Nikawaambia, “Mkiona kuwa ni vyema, nipeni ujira wangu, la sivyo, basi msinipe.” Kwa hiyo wakanilipa vipande thelathini vya fedha.
13
Naye Bwana akaniambia, “Mtupie mfinyanzi,” hiyo bei nzuri waliyonithaminia! Kwa hiyo nikachukua hivyo vipande thelathini vya fedha na kumtupia huyo mfinyanzi katika nyumba ya Bwana.
14
Kisha nikaivunja fimbo yangu ya pili iitwayo Umoja, kuvunja undugu kati ya Yuda na Israeli!

Kuwasili kwa Mchungaji Asiyefaa

15
Kisha Bwana akaniambia, “Vitwae tena vifaa vya mchungaji mpumbavu.
16
Kwa maana ninakwenda kumwinua mchungaji juu ya nchi ambaye hatamjali aliyepotea, wala kuwatafuta wale wachanga au kuwaponya waliojeruhiwa, wala kuwalisha wenye afya, lakini atakula nyama ya kondoo wanono na kuzirarua kwato zao.
17
“Ole wa mchungaji asiyefaa, anayeliacha kundi! Upanga na uupige mkono wake na jicho lake la kuume! Mkono wake na unyauke kabisa, jicho lake la kuume lipofuke kabisa!”
Use arrow keys to navigate
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Reading Width 45 chars

Options