Wimbo2
Listen to this chapter
0:00
0:00
Tamko la Upendo la Mshulami
1
Mimi ni ua la Sharoni, yungiyungi ya bondeni.
2
Kama yungiyungi katikati ya miiba ndivyo alivyo mpenzi wangu katikati ya wanawali.
Ubora wa Mpendwa
3
Kama mti wa mtofaa miongoni mwa miti ya msituni ndivyo alivyo mpenzi wangu miongoni mwa wanaume vijana. Ninafurahia kuketi kivulini mwa mwanaume huyu, na tunda lake ni tamu kwangu.
4
Amenichukua mpaka kwenye ukumbi wa karamu, na bendera ya huyu mwanaume juu yangu ni upendo.
5
Nitie nguvu kwa zabibu kavu, niburudishe kwa matofaa, kwa maana ninazimia kwa mapenzi.
6
Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu, na mkono wake wa kuume unanikumbatia.
7
Binti za Yerusalemu, ninawaagiza kwa paa na kwa ayala wa shambani: Msichochee wala kuamsha mapenzi hata yatakapotaka yenyewe.
Kufika kwa Mpendwa
8
Sikiliza! Mpenzi wangu! Tazama! Huyu hapa anakuja, akirukaruka juu milimani akizunguka juu ya vilima.
9
Mpenzi wangu ni kama paa au ayala kijana. Tazama! Anasimama nyuma ya ukuta wetu, akitazama kupitia madirishani, akichungulia kimiani.
Mwito wa Upendo
10
Mpenzi wangu alizungumza na kuniambia, “Inuka, mpenzi wangu, mrembo wangu, tufuatane.
11
Tazama! Wakati wa masika umepita, mvua imekwisha na ikapita.
12
Maua yanatokea juu ya nchi; majira ya kuimba yamewadia, sauti za njiwa zinasikika katika nchi yetu.
13
Mtini unatunga matunda yake ya mwanzoni, zabibu zinazochanua zaeneza harufu nzuri. Inuka, njoo mpenzi wangu. Mrembo wangu, tufuatane.”
Ombi la Ukaribu
14
Hua wangu penye nyufa za majabali, mafichoni pembezoni mwa mlima, nionyeshe uso wako, na niisikie sauti yako, kwa maana sauti yako ni tamu, na uso wako unapendeza.
Kulinda Mashamba ya Mizabibu ya Upendo
15
Tukamatie mbweha, mbweha wale wadogo wanaoharibu mashamba ya mizabibu, mashamba yetu ya mizabibu yaliyochanua.
Kumiliki na Kufurahia kwa Pande Zote
16
Mpenzi wangu ni wangu, nami ni wake, yeye hujilisha katikati ya yungiyungi.
Kutarajia Kuungana Tena
17
Mpaka jua linapochomoza, na vivuli vikimbie, rudi, mpenzi wangu, na uwe kama paa, au kama ayala kijana juu ya vilima vya Betheri.
Use ← → arrow keys to navigate
Settings
Reading Style
Typeface
Font Size px
Reading Width chars
Options
Study Note