God
Mistari inayomtaja God
Nyuma ya milango yako na miimo yako umeweka alama zako za kipagani. Kwa kuniacha mimi, ulifunua kitanda chako, umepanda juu yake na kukipanua sana; ulifanya patano na wale ambao unapenda vitanda vyao, nawe uliangalia uchi wao.
“Ni nani uliyemhofu hivyo na kumwogopa hata ukawa mwongo kwangu, wala hukunikumbuka au kutafakari hili moyoni mwako? Si ni kwa sababu nimekuwa kimya muda mrefu hata huniogopi?
Nitaifunua haki yako na matendo yako, nayo hayatakufaidi.
Utakapolia kwa kuhitaji msaada, sanamu zako ulizojikusanyia na zikuokoe! Upepo utazipeperusha zote, pumzi peke yake itazipeperusha, Lakini mtu atakayenifanya kimbilio lake, atairithi nchi na kuumiliki mlima wangu mtakatifu.”
Tena itasemwa: “Jengeni, jengeni, itengenezeni njia! Ondoeni vikwazo katika njia ya watu wangu.”
Kwa maana hili ndilo asemalo Aliye juu, yeye aliyeinuliwa sana, yeye aishiye milele, ambaye jina lake ni Mtakatifu: “Ninaishi mimi mahali palipoinuka na patakatifu, lakini pia pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na mwenye roho ya unyenyekevu, ili kuzihuisha roho za wanyenyekevu na kuihuisha mioyo yao waliotubu.
Sitaendelea kulaumu milele, wala sitakasirika siku zote, kwa kuwa roho ya mwanadamu ingezimia mbele zangu: yaani pumzi ya mwanadamu niliyemuumba.
Nilighadhibika na tamaa yake ya dhambi; nilimwadhibu, nikauficha uso wangu kwa hasira, na bado aliendelea katika njia zake za tamaa.
Nimeziona njia zake, lakini nitamponya, nitamwongoza na kumrudishia upya faraja,
nikiumba sifa midomoni ya waombolezaji katika Israeli. Amani, amani, kwa wale walio mbali na kwa wale walio karibu,” asema Bwana. “Nami nitawaponya.”
Mungu wangu asema, “Hakuna amani kwa waovu.”
“Piga kelele, usizuie. Paza sauti yako kama tarumbeta. Watangazieni watu wangu uasi wao, na kwa nyumba ya Yakobo dhambi zao.
Kwa maana kila siku hunitafuta, wanaonekana kutaka kujua njia zangu, kana kwamba walikuwa taifa linalotenda lililo sawa, na ambalo halijaziacha amri za Mungu wake. Hutaka kwangu maamuzi ya haki, nao hutamani Mungu awakaribie.
Je, hii ndiyo aina ya mfungo niliouchagua, siku moja tu ya mtu kujinyenyekeza? Je, ni kwa kuinamisha kichwa chini kama tete, na kwa kujilaza juu ya nguo ya gunia na majivu? Je, huo ndio mnaouita mfungo, siku iliyokubalika kwa Bwana?
“Je, hii si ndiyo aina ya mfungo niliyoichagua: kufungua minyororo ya udhalimu, na kufungua kamba za nira, kuwaweka huru walioonewa, na kuvunja kila nira?
Ndipo nuru yako itajitokeza kama mapambazuko na uponyaji wako utatokea upesi; ndipo haki yako itakapokutangulia mbele yako, na utukufu wa Bwana utakuwa mlinzi nyuma yako.
Ndipo utaita, naye Bwana atajibu, utalia kuomba msaada, naye atasema: Mimi hapa. “Kama ukiiondoa nira ya udhalimu, na kunyoosha kidole na kuzungumza maovu,
Bwana atakuongoza siku zote, atayatosheleza mahitaji yako katika nchi kame, naye ataitia nguvu mifupa yako. Utakuwa kama bustani iliyonyweshwa vizuri, kama chemchemi ambayo maji yake hayakauki kamwe.
“Kama ukitunza miguu yako isivunje Sabato, na kutokufanya kama vile upendavyo katika siku yangu takatifu, kama ukiita Sabato siku ya furaha na siku takatifu ya Bwana ya kuheshimiwa, kama utaiheshimu kwa kutoenenda katika njia zako mwenyewe, na kutokufanya yakupendezayo au kusema maneno ya upuzi,
ndipo utakapojipatia furaha yako katika Bwana, nami nitakufanya upande juu ya miinuko ya nchi na kusherehekea urithi wa Yakobo baba yako.” Kinywa cha Bwana kimenena haya.
Hakika mkono wa Bwana si mfupi hata usiweze kuokoa, wala sikio lake si zito hata lisiweze kusikia.
Lakini maovu yenu yamewatenga ninyi na Mungu wenu, dhambi zenu zimewaficha ninyi uso wake, ili asisikie.
Kwa sababu makosa yetu ni mengi machoni pako, na dhambi zetu zinashuhudia dhidi yetu. Makosa yetu yako pamoja nasi daima, nasi tunayatambua maovu yetu:
Uasi na udanganyifu dhidi ya Bwana, kumgeuzia Mungu wetu kisogo, tukichochea udhalimu na maasi, tukinena uongo ambao mioyo yetu imeuhifadhi.
Kweli haipatikani popote, na yeyote aepukaye uovu huwa mawindo. Bwana alitazama naye akachukizwa kwamba hapakuwepo haki.