Mathayo 12:6-30
6
Nawaambia wazi kwamba, yeye aliye mkuu kuliko Hekalu yupo hapa.
7
Kama mngekuwa mmejua maana ya maneno haya, ‘Nataka rehema, wala si dhabihu,’ msingewalaumu watu wasio na hatia,
8
kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”
9
Yesu akaondoka mahali hapo, akaingia ndani ya sinagogi lao,
10
na huko alikuwepo mtu aliyepooza mkono. Wakitafuta sababu ya kumshtaki Yesu, wakamuuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?”
11
Yesu akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu, mwenye kondoo wake ambaye huyo kondoo akitumbukia shimoni siku ya Sabato hatamtoa?
12
Mtu ana thamani kubwa kuliko kondoo. Kwa hiyo ni halali kutenda mema siku ya Sabato.”
13
Ndipo akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa ukawa mzima kama ule mwingine.
14
Lakini Mafarisayo wakatoka nje, wakafanya shauri baya juu ya Yesu jinsi watakavyoweza kumuua.
15
Lakini Yesu alipoyatambua mawazo yao, akaondoka mahali hapo. Watu wengi wakamfuata, naye akawaponya wagonjwa wao wote,
16
akiwakataza wasiseme yeye ni nani.
17
Hii ilikuwa ili litimie lile neno lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya kusema:
18
“Tazama mtumishi wangu niliyemchagua, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Nitaweka Roho wangu juu yake, naye atatangaza haki kwa mataifa.
19
Hatagombana wala hatapiga kelele, wala hakuna atakayesikia sauti yake njiani.
20
Mwanzi uliopondeka hatauvunja, na utambi unaofuka moshi hatauzima, mpaka atakapoifanya haki ishinde.
21
Katika Jina lake mataifa wataweka tumaini lao.”
22
Kisha wakamletea mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, na alikuwa kipofu na bubu. Yesu akamponya, hata akaweza kusema na kuona.
23
Watu wote wakashangaa na kusema, “Je, yawezekana huyu ndiye Mwana wa Daudi?”
24
Lakini Mafarisayo waliposikia jambo hili wakasema, “Mtu huyu anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo wachafu.”
25
Yesu alijua walichokuwa wakiwaza, hivyo akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Hali kadhalika kila mji au watu wa nyumba moja waliogawanyika dhidi yao wenyewe hawawezi kusimama.
26
Kama Shetani akimtoa Shetani, atakuwa amegawanyika yeye mwenyewe. Basi ufalme wake utawezaje kusimama?
27
Nami kama natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, watu wenu je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu.
28
Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa Roho wa Mungu, basi Ufalme wa Mungu umekuja juu yenu.
29
“Au tena, mtu awezaje kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Akishamfunga, ndipo hakika anaweza kuteka nyara mali zake.
30
“Mtu asiyekuwa pamoja nami yu kinyume nami, na mtu ambaye hakusanyi pamoja nami, hutawanya.
Settings