Waamuzi 8:16-35
16
Akawachukua hao viongozi wa mji na kuwafundisha watu wa Sukothi somo kwa kuwaadhibu kwa miiba na michongoma ya nyikani.
17
Pia akaubomoa mnara wa Penieli na kuwaua watu wa mji.
18
Kisha akawauliza Zeba na Salmuna, “Ni watu wa aina gani mliowaua huko Tabori?” Wakajibu, “Ni watu kama wewe, kila mmoja wao akiwa na nafasi ya uana wa mfalme.”
19
Gideoni akajibu, “Hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mama yangu hasa. Hakika kama aishivyo Bwana, kama mngekuwa mmewaacha hai, mimi nisingewaua ninyi.”
20
Akamgeukia Yetheri, mwanawe mzaliwa wa kwanza, akasema, “Waue hawa!” Lakini Yetheri hakuufuta upanga wake, kwa sababu aliogopa, kwa kuwa alikuwa bado kijana mdogo tu.
21
Zeba na Salmuna wakasema, “Njoo ufanye hivyo wewe mwenyewe. ‘Alivyo mtu, ndivyo zilivyo nguvu zake.’ ” Hivyo Gideoni akatoka mbele na kuwaua, naye akayaondoa mapambo kwenye shingo za ngamia zao.
22
Waisraeli wakamwambia Gideoni, “Ututawale, wewe, wanao na wana wa wana wako, kwa kuwa umetuokoa kutoka mikononi mwa Wamidiani.”
23
Lakini Gideoni akawaambia, “Mimi sitatawala juu yenu, wala wanangu hawatatawala juu yenu. Bwana ndiye atakayetawala juu yenu ninyi.”
24
Naye akasema, “Ninalo ombi moja, kwamba kila mmoja wenu anipatie kipuli kutoka kwenye fungu lake la nyara.” (Ilikuwa desturi ya Waishmaeli kuvaa vipuli vya dhahabu.)
25
Wakajibu, “Tutafurahi kuvitoa.” Hivyo wakatanda vazi chini na kila mwanaume akatupia juu yake pete kutoka kwenye fungu lake la nyara.
26
Uzito wa pete za dhahabu alizoomba zilifikia shekeli 1,700, bila kuhesabu mapambo mengine, pete za masikio na mavazi ya zambarau yaliyovaliwa na wafalme wa Midiani, au mikufu iliyokuwa kwenye shingo za ngamia zao.
27
Gideoni akatengeneza kisibau kwa kutumia ile dhahabu, ambacho alikiweka katika mji wake, yaani, Ofra. Waisraeli wote wakafanya uasherati kwa kukiabudu huko, nacho kikawa mtego kwa Gideoni na jamaa yake.
28
Hivyo Midiani ikashindwa mbele ya Israeli nayo haikuinua kichwa chake tena. Wakati wa siku za uhai wa Gideoni, nchi ikafurahia amani miaka arobaini.
29
Yerub-Baali mwana wa Yoashi akarudi kwenda kuishi katika nyumba yake.
30
Alikuwa na wana sabini wa kwake mwenyewe, kwa kuwa alikuwa na wake wengi.
31
Suria wake, aliyekuwa anaishi huko Shekemu, pia alimzalia mwana, ambaye alimwita Abimeleki.
32
Gideoni mwana wa Yoashi akafa akiwa na umri mzuri wa uzee, na akazikwa katika kaburi la Yoashi baba yake huko Ofra ya Waabiezeri.
33
Mara tu alipofariki Gideoni, Waisraeli wakarudia hali ya uovu na kufanya uasherati kwa kuabudu Mabaali. Wakamsimamisha Baal-Berithi kuwa mungu wao na
34
wala hawakumkumbuka Bwana Mungu wao, aliyewaokoa kutoka mikononi mwa adui zao wote kutoka kila upande.
35
Pia wakashindwa kuitendea mema jamaa ya Yerub-Baali (yaani Gideoni) kwa ajili ya mambo yote mema aliyokuwa amefanya kwa ajili yao.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings