Yoshua 7:1-12
1
Lakini Waisraeli hawakuwa waaminifu kuhusu vile vitu vilivyowekwa wakfu; Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, alivichukua baadhi ya hivyo vitu. Hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Israeli.
2
Basi Yoshua akatuma watu kutoka Yeriko waende Ai, karibu na Beth-Aveni mashariki ya Betheli, akawaambia, “Pandeni mkaipeleleze nchi.” Basi wale watu wakapanda wakaipeleleza Ai.
3
Waliporudi kwa Yoshua, wakasema, “Si lazima watu wote waende kupigana na Ai. Watume watu elfu mbili au tatu wakauteke huo mji. Usiwachoshe watu wote, kwa sababu huko kuna watu wachache tu.”
4
Basi wakapanda kama watu elfu tatu tu, lakini wakashambuliwa na watu wa Ai,
5
ambao waliwaua watu kama thelathini na sita miongoni mwao. Wakawafukuza Waisraeli kutoka lango la mji hadi Shebarimu, nao wakawauwa huko kwenye materemko. Kutokana na hili mioyo ya watu ikayeyuka ikawa kama maji.
6
Ndipo Yoshua akayararua mavazi yake, akaanguka kifudifudi mbele ya Sanduku la Bwana, na akabakia hapo mpaka jioni. Wazee wa Israeli nao wakafanya vivyo hivyo wakatia mavumbi vichwani mwao.
7
Yoshua akasema, “Ee Bwana Mwenyezi, kwa nini umewavusha watu hawa ngʼambo ya Yordani ili kututia mikononi mwa Waamori watuangamize? Laiti tungeliridhika kukaa ngʼambo ile nyingine ya Yordani!
8
Ee Bwana, niseme nini sasa, ikiwa sasa Israeli ameshafukuzwa na adui zake?
9
Wakanaani na watu wengine wa nchi watasikia habari hii, nao watatuzunguka na kutufutilia jina letu duniani. Utafanya nini basi kwa ajili ya jina lako mwenyewe lililo kuu?”
10
Bwana akamwambia Yoshua, “Simama! Unafanya nini hapo chini kifudifudi?
11
Israeli ametenda dhambi. Wamekiuka agano langu nililowaamuru kulishika. Wamechukua baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu, wameiba, wamesema uongo, wameviweka pamoja na mali zao.
12
Ndiyo sababu Waisraeli hawawezi kusimama dhidi ya adui zao. Wanawapa visogo na kukimbia kwa kuwa wanastahili maangamizi. Sitakuwa pamoja nanyi tena mpaka mwangamize kila kitu miongoni mwenu kilichotengwa kwa maangamizi.
Settings