Yeremia 49:1-22
1
Kuhusu Waamoni: Hili ndilo asemalo Bwana: “Je, Israeli hana wana? Je, hana warithi? Kwa nini basi Moleki amechukua milki ya Gadi? Kwa nini watu wake wanaishi katika miji yake?
2
Lakini siku zinakuja,” asema Bwana, “nitakapopiga kelele ya vita dhidi ya Raba mji wa Waamoni; utakuwa kilima cha magofu, navyo vijiji vinavyouzunguka vitateketezwa kwa moto. Kisha Israeli atawafukuza wale waliomfukuza,” asema Bwana.
3
“Lia kwa huzuni, ee Heshboni, kwa kuwa Ai umeangamizwa! Pigeni kelele, enyi wakazi wa Raba! Vaeni nguo za gunia na kuomboleza, kimbieni hapa na pale ndani ya kuta, kwa kuwa Moleki atakwenda uhamishoni, yeye pamoja na makuhani na maafisa wake.
4
Kwa nini unajivunia mabonde yako, kujivunia mabonde yako yaliyozaa sana? Ee binti usiye mwaminifu, unayeutumainia utajiri wako na kusema, ‘Ni nani atakayenishambulia?’
5
Nitaleta hofu kuu juu yako kutoka kwa wale wote wanaokuzunguka,” asema Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote. “Kila mmoja wenu ataondolewa, wala hakuna hata mmoja atakayekusanya wakimbizi.
6
“Lakini hatimaye, nitarudisha mateka wa Waamoni,” asema Bwana.
7
Kuhusu Edomu: Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Je, hakuna tena hekima katika Temani? Je, shauri limewapotea wenye busara? Je, hekima yao imechakaa?
8
Geuka na ukimbie, jifiche katika mapango marefu kabisa, wewe uishiye Dedani, kwa kuwa nitaleta maafa juu ya Esau wakati nitakapomwadhibu.
9
Je, kama wachuma zabibu wangekuja kwako, wasingebakiza zabibu chache? Kama wezi wangekujia usiku, je, si wangeiba tu kiasi ambacho wangehitaji?
10
Lakini nitamvua Esau nguo abaki uchi, nitayafunua maficho yake, ili asiweze kujificha. Watoto wake, jamaa na majirani wataangamia, naye hatakuwepo tena.
11
Waache yatima wako; nitayalinda maisha yao. Wajane wako pia wanaweza kunitumaini mimi.”
12
Hili ndilo asemalo Bwana: “Kama wale wasiostahili kukinywea kikombe ni lazima wakinywe, kwa nini wewe usiadhibiwe? Hutakwepa kuadhibiwa, ni lazima ukinywe.
13
Ninaapa kwa nafsi yangu,” asema Bwana, “kwamba Bosra utakuwa magofu na kitu cha kutisha, cha aibu na cha kulaania; miji yake yote itakuwa magofu milele.”
14
Nimesikia ujumbe kutoka kwa Bwana: Mjumbe alitumwa kwa mataifa kusema, “Jikusanyeni ili kuushambulia! Inukeni kwa ajili ya vita!”
15
“Sasa nitakufanya uwe mdogo miongoni mwa mataifa, aliyedharauliwa miongoni mwa watu.
16
Vitisho vyako na kiburi cha moyo wako vimekudanganya, wewe unayeishi katika majabali ya miamba, wewe unayedumu katika miinuko ya kilima. Ujapojenga kiota chako juu sana kama cha tai, nitakushusha chini kutoka huko,” asema Bwana.
17
“Edomu atakuwa kitu cha kuogofya; wote wapitao karibu watashangaa na kuzomea kwa sababu ya majeraha yake yote.
18
Kama vile Sodoma na Gomora zilivyoangamizwa, pamoja na miji iliyokuwa jirani nayo,” asema Bwana, “vivyo hivyo hakuna mtu yeyote atakayeishi humo. Naam, hakuna mtu yeyote atakayekaa humo.
19
“Kama simba anayepanda kutoka vichaka vya Yordani kuja kwenye nchi ya malisho mengi, ndivyo nitamfukuza Edomu kutoka nchi yake ghafula. Ni nani aliye mteule nitakayemweka kwa ajili ya jambo hili? Ni nani aliye kama mimi, na ni nani awezaye kunipinga? Tena ni mchungaji yupi awezaye kusimama kinyume nami?”
20
Kwa hiyo, sikia kile Bwana alichokipanga dhidi ya Edomu, kile alichokusudia dhidi ya wale waishio Temani: Aliye mchanga katika kundi ataburutwa mbali; yeye ataharibu kabisa malisho yao kwa sababu yao.
21
Kwa sauti ya anguko lao, dunia itatetemeka. Kilio chao kitasikika hadi Bahari ya Shamu.
22
Tazama! Tai atapaa juu angani na kuruka chini kwa ghafula, akitandaza mabawa yake juu ya Bosra. Katika siku hiyo, mioyo ya mashujaa wa Edomu itakuwa kama moyo wa mwanamke katika utungu wa kuzaa.
Settings