Skip to content
Yeremia 44:15-28

Yeremia 44:15-28

15
Kisha wanaume wote ambao walijua kwamba wake zao walikuwa wakifukiza uvumba kwa miungu mingine, pamoja na wanawake wote waliokuwako, yaani, kusanyiko kubwa na watu wote walioishi nchi ya Misri na Pathrosi, wakamwambia Yeremia,
16
“Hatutausikiliza ujumbe uliotuambia katika jina la Bwana!
17
Hakika tutafanya kila kitu tulichosema tutakifanya: Tutafukiza uvumba kwa Malkia wa Mbinguni na tutammiminia sadaka zetu za kinywaji kama vile sisi na baba zetu, wafalme wetu na maafisa wetu tulivyofanya katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu. Wakati ule tulikuwa na chakula tele, tulikuwa matajiri wala hatukupata dhara lolote.
18
Lakini tangu tulipoacha kumfukizia uvumba Malkia wa Mbinguni na kummiminia sadaka za kinywaji, hatupati chochote, na tumekuwa tukiangamizwa kwa upanga na njaa.”
19
Wanawake wakaongeza kusema, “Wakati tulipomfukizia uvumba Malkia wa Mbinguni na kummiminia sadaka zetu za kinywaji, je, waume zetu hawakujua kwamba tulikuwa tukitengeneza maandazi kwa mfano wake, na kummiminia yeye sadaka za kinywaji?”
20
Ndipo Yeremia akawaambia watu wote, wanaume na wanawake waliokuwa wakimjibu,
21
“Je, Bwana hakukumbuka na kufikiri juu ya uvumba uliofukizwa katika miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu na ninyi pamoja na baba zenu, wafalme wenu, maafisa wenu na watu wa nchi?
22
Bwana alipokuwa hawezi kuendelea kuvumilia matendo yenu maovu na mambo ya machukizo mliyoyafanya, nchi yenu ilikuwa kitu cha kulaania na kuachwa ukiwa pasipo wakazi, kama ilivyo leo.
23
Kwa sababu mmefukiza uvumba na kufanya dhambi dhidi ya Bwana, nanyi hamkumtii wala kufuata sheria yake au amri zake au maagizo yake, maafa haya yamekuja juu yenu, kama mnavyoona sasa.”
24
Kisha Yeremia akawaambia watu wote, pamoja na wanawake, “Sikieni neno la Bwana, enyi watu wote wa Yuda mlioko Misri.
25
Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Ninyi na wake zenu mmeonyesha kwa matendo yenu kile mlichoahidi mliposema, ‘Hakika tutatimiza nadhiri tulizoziweka za kumfukizia uvumba na kummiminia sadaka za kinywaji Malkia wa Mbinguni.’ “Endeleeni basi, fanyeni yale mliyoahidi! Timizeni nadhiri zenu!
26
Lakini sikieni neno la Bwana, enyi Wayahudi wote mnaoishi Misri: ‘Ninaapa kwa Jina langu lililo kuu,’ asema Bwana, ‘kwamba hakuna hata mmoja atokaye Yuda anayeishi popote Misri ambaye kamwe ataomba tena kwa Jina langu au kuapa, akisema, “Hakika kama Bwana Mwenyezi aishivyo.”
27
Kwa maana ninawaangalia kwa ajili ya madhara, wala sio kwa mema. Wayahudi walioko Misri wataangamia kwa upanga na njaa, hadi wote watakapoangamizwa.
28
Wale watakaonusurika upanga na kurudi katika nchi ya Yuda kutoka Misri watakuwa wachache sana. Ndipo mabaki wote wa Yuda waliokuja kuishi Misri watakapojua ni neno la nani litakalosimama, kwamba ni langu au lao.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options