Skip to content
Yeremia 44:1-14

Yeremia 44:1-14

1
Neno hili lilimjia Yeremia kuhusu Wayahudi wote waishio Misri, huko Migdoli, Tahpanhesi na Memfisi, katika nchi ya Pathrosi kusema:
2
“Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Mliona maangamizi makubwa niliyoyaleta juu ya Yerusalemu na juu ya miji yote ya Yuda. Leo imeachwa ukiwa na magofu
3
kwa sababu ya uovu waliokuwa wameufanya. Walinikasirisha kwa kufukiza uvumba na kwa kuabudu miungu mingine ambayo kamwe wao, wala ninyi, wala baba zenu hawakuifahamu.
4
Tena na tena, niliwatuma watumishi wangu manabii ambao walisema, ‘Msifanye jambo hili la kuchukiza ambalo nalichukia!’
5
Lakini hawakusikiliza wala hawakujali, hawakugeuka ili kuuacha uovu wao, wala hawakuacha kufukiza uvumba kwa miungu mingine.
6
Kwa hiyo hasira yangu kali ilimwagika, ikawaka dhidi ya miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu, na kuifanya ukiwa na magofu kama ilivyo leo.
7
“Basi hili ndilo Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Kwa nini kujiletea maafa makubwa kama haya juu yenu kwa kujikatilia mbali kutoka Yuda wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, hata kujiacha bila mabaki?
8
Kwa nini kuichochea hasira yangu kwa kile ambacho mikono yenu imekitengeneza, mkaifukizia uvumba miungu mingine huko Misri, mahali mlipokuja kuishi? Mtajiangamiza wenyewe na kujifanya kitu cha kulaania na shutumu miongoni mwa mataifa yote duniani.
9
Je, mmesahau uovu uliotendwa na baba zenu, na wafalme na malkia wa Yuda, na uovu uliofanywa na ninyi na wake zenu katika nchi ya Yuda na barabara za Yerusalemu?
10
Mpaka leo hawajajinyenyekeza au kuonyesha heshima, wala hawajafuata sheria yangu na amri nilizoweka mbele yenu na baba zenu.
11
“Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Mimi nimekusudia kuleta maafa juu yenu, na kuiangamiza Yuda yote.
12
Nitawaondoa mabaki ya Yuda waliokusudia kwenda Misri kukaa humo. Wote wataangamia huko Misri, wataanguka kwa upanga au kufa kwa njaa. Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana, watakufa kwa upanga au njaa. Watakuwa kitu cha kulaania na cha kutisha, cha laumu na shutumu.
13
Nitawaadhibu wale waishio Misri kwa upanga, njaa na tauni kama nilivyoiadhibu Yerusalemu.
14
Hakuna hata mmoja wa mabaki ya Yuda ambaye amekwenda kuishi Misri atakayeepuka au kunusurika ili kurudi katika nchi ya Yuda, ambayo wanaitamani sana kurudi na kuishi ndani yake, hakuna hata mmoja atakayerudi isipokuwa wakimbizi wachache.”
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options