Yeremia 22:1-19
1
Hili ndilo asemalo Bwana: “Shuka kwenye jumba la kifalme la mfalme wa Yuda, utangaze ujumbe huu huko:
2
‘Sikia neno la Bwana, ee mfalme wa Yuda, wewe uketiye kwenye kiti cha enzi cha Daudi: wewe, maafisa wako na watu wako mnaopitia malango haya.
3
Hili ndilo Bwana asemalo: Tenda haki na adili. Mwokoe mkononi mwa mdhalimu yeye aliyetekwa nyara. Usimtendee mabaya wala ukatili mgeni, yatima au mjane, wala usimwage damu isiyo na hatia mahali hapa.
4
Kwa kuwa ukiwa mwangalifu kushika maagizo haya, ndipo wafalme watakaokalia kiti cha enzi cha Daudi watakapoingia kupitia malango ya jumba hili la kifalme, wakiwa wamepanda magari na farasi, huku wakifuatana na maafisa wao na watu wao.
5
Lakini kama hutayatii maagizo haya, asema Bwana, ninaapa kwa nafsi yangu kwamba jumba hili litakuwa gofu.’ ”
6
Kwa kuwa hili ndilo Bwana asemalo kuhusu jumba la kifalme la mfalme wa Yuda: “Ingawa uko kama Gileadi kwangu, kama kilele cha Lebanoni, hakika nitakufanya uwe kama jangwa, kama miji ambayo haijakaliwa na watu.
7
Nitawatuma waharabu dhidi yako, kila mtu akiwa na silaha zake, nao watazikata boriti zako nzuri za mierezi na kuzitupa motoni.
8
“Watu kutoka mataifa mengi watapitia karibu na mji huu na kuulizana, ‘Kwa nini Bwana amefanya jambo la namna hii juu ya mji huu mkubwa?’
9
Nalo jibu litakuwa: ‘Kwa sababu wameliacha agano la Bwana, Mungu wao, na wameabudu na kuitumikia miungu mingine.’ ”
10
Usimlilie yeye aliyekufa, wala usimwombolezee; badala yake, afadhali umlilie kwa uchungu yule aliyepelekwa uhamishoni, kwa sababu kamwe hatairudia wala kuiona tena nchi yake alikozaliwa.
11
Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana kuhusu Shalumu mwana wa Yosia, aliyeingia mahali pa baba yake kuwa mfalme wa Yuda, lakini ameondoka mahali hapa: “Yeye kamwe hatarudi tena.
12
Atafia huko mahali walipompeleka kuwa mateka; hataiona tena nchi hii.”
13
“Ole wake yeye ajengaye jumba lake la kifalme kwa njia ya dhuluma, vyumba vyake vya juu kwa udhalimu, akiwatumikisha watu wa nchi yake pasipo malipo, bila kuwalipa kwa utumishi wao.
14
Asema, ‘Nitajijengea jumba kuu la kifalme, na vyumba vya juu vyenye nafasi kubwa.’ Hivyo anaweka ndani yake madirisha makubwa, huweka kuta za mbao za mierezi, na kuipamba kwa rangi nyekundu.
15
“Je, inakufanya kuwa mfalme huko kuongeza idadi ya mierezi? Je, baba yako hakuwa na chakula na kinywaji? Alifanya yaliyo sawa na haki, hivyo yeye akafanikiwa katika yote.
16
Aliwatetea maskini na wahitaji, hivyo yeye akafanikiwa katika yote. Je, hiyo si ndiyo maana ya kunijua mimi?” asema Bwana.
17
“Lakini macho yako na moyo wako vimeelekezwa tu katika mapato ya udhalimu, kwa kumwaga damu isiyo na hatia, kwa uonevu na ukatili.”
18
Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana kuhusu Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda: “Hawatamwombolezea wakisema: ‘Ole, ndugu yangu! Ole, umbu langu!’ Hawatamwombolezea wakisema: ‘Ole, bwana wangu! Ole, fahari yake!’
19
Atazikwa maziko ya punda: ataburutwa na kutupwa nje ya malango ya Yerusalemu.”
Settings