Skip to content
Isaya 30:1-17

Isaya 30:1-17

1
Bwana asema, “Ole kwa watoto wakaidi, kwa wale wanaotimiza mipango ambayo si yangu, wakifanya makubaliano, lakini si kwa Roho wangu, wakilundika dhambi juu ya dhambi,
2
wale washukao kwenda Misri bila kutaka shauri langu, wanaotafuta msaada wa ulinzi wa Farao, watafutao kivuli cha Misri kwa ajili ya kimbilio.
3
Lakini ulinzi wa Farao utakuwa kwa aibu yenu, kivuli cha Misri kitawaletea fedheha.
4
Ingawa wana maafisa katika Soani na wajumbe wamewasili katika Hanesi,
5
kila mmoja ataaibishwa kwa sababu ya taifa lisilowafaa kitu, ambalo haliwaletei msaada wala faida, bali aibu tu na fedheha.”
6
Neno kuhusu wanyama wa Negebu: Katika nchi ya taabu na shida, ya simba za dume na jike, ya nyoka mwenye sumu kali na nyoka warukao, wajumbe huchukua utajiri wao juu ya migongo ya punda, hazina zao juu ya nundu za ngamia, kwa lile taifa lisilokuwa na faida,
7
kuvipeleka Misri, ambaye msaada wake haufai kabisa. Kwa hiyo nimemwita “Rahabu Asiyefanya Chochote.”
8
Nenda sasa, liandike neno hili juu ya kibao kwa ajili yao, liandike kwenye kitabu, ili liweze kuwa shahidi milele kwa ajili ya siku zijazo.
9
Hawa ni watu waasi, watoto wadanganyifu, watoto ambao hawataki kusikiliza mafundisho ya Bwana.
10
Wanawaambia waonaji, “Msione maono tena!” Nako kwa manabii wanasema, “Msiendelee kutupatia maono ambayo ni ya kweli! Tuambieni mambo ya kupendeza, tabirini mambo ya uongo.
11
Acheni njia hii, ondokeni katika mapito haya, nanyi acheni kutukabili pamoja na yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli!”
12
Kwa hiyo, hili ndilo asemalo yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli: “Kwa sababu mmekataa ujumbe huu, mkategemea uonevu na kutumainia udanganyifu,
13
dhambi hii itakuwa kwenu kama ukuta mrefu, wenye ufa na wenye kubetuka, ambao unaanguka ghafula, mara moja.
14
Utavunjika vipande vipande kama chombo cha udongo ukipasuka pasipo huruma ambapo katika vipande vyake hakuna kipande kitakachopatikana kwa kuukulia makaa kutoka jikoni au kuchotea maji kisimani.”
15
Hili ndilo Bwana Mwenyezi, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, asemalo: “Katika kutubu na kupumzika ndio wokovu wenu, katika kutulia na kutumaini ndizo nguvu zenu, lakini hamkutaka.
16
Mlisema, ‘Hapana, tutakimbia kwa farasi.’ Kwa hiyo mtakimbia! Mlisema, ‘Tutakimbia kwa farasi waendao kasi.’ Kwa hiyo wanaowafukuza watakwenda kasi!
17
Watu 1,000 watakimbia kwa ajili ya kitisho cha mtu mmoja, kwa vitishio vya watu watano wote mtakimbia, hadi mtakapoachwa kama mlingoti wa bendera juu ya kilele cha mlima, kama bendera juu ya kilima.”
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options