Skip to content
Isaya 28:1-15

Isaya 28:1-15

1
Ole kwa lile taji la maua, kiburi cha walevi wa Efraimu, kwa ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake, uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba: kwa ule mji, kiburi cha wale walioshushwa na mvinyo!
2
Tazama, Bwana anaye mmoja aliye na uwezo na nguvu. Kama dhoruba ya mvua ya mawe na upepo uharibuo, kama mvua inyeshayo kwa nguvu na mafuriko yashukayo, atakiangusha chini kwa nguvu.
3
Lile taji la maua, kiburi cha walevi cha Efraimu, kitakanyagwa chini ya nyayo.
4
Lile ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake, uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba, litakuwa kama tini iliyoiva kabla ya mavuno: mara mtu aionapo, huichuma na kuila.
5
Katika siku ile, Bwana Mwenye Nguvu Zote atakuwa taji la utukufu, taji zuri la maua kwa mabaki ya watu wake.
6
Atakuwa roho ya haki kwa yeye aketiye katika kiti cha hukumu, chanzo cha nguvu kwa wale wazuiao vita langoni.
7
Hawa pia wanapepesuka kwa sababu ya mvinyo, wanayumbayumba kwa sababu ya kileo: Makuhani na manabii wanapepesuka kwa sababu ya kileo, wanachanganyikiwa kwa sababu ya mvinyo; wanapepesuka wanapoona maono, wanajikwaa wanapotoa maamuzi.
8
Meza zote zimejawa na matapishi wala hakuna sehemu hata ndogo isiyokuwa na uchafu.
9
“Yeye anajaribu kumfundisha nani? Yeye anamwelezea nani ujumbe wake? Je, ni kwa watoto walioachishwa kunyonya? Je, ni wale ambao ndipo tu wametolewa matitini?
10
Kwa maana ni: Amri juu ya amri, amri juu ya amri, kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni; hapa kidogo, kule kidogo.”
11
Sawa kabisa, kwa midomo migeni na kwa lugha ngeni, Mungu atasema na watu hawa,
12
wale ambao aliwaambia, “Hapa ni mahali pa kupumzika, waliochoka na wapumzike,” na, “Hapa ni mahali pa mapumziko,” lakini hawakutaka kusikiliza.
13
Hivyo basi, neno la Bwana kwao litakuwa: Amri juu ya amri, amri juu ya amri, kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni, hapa kidogo, kule kidogo: ili waende na kuanguka chali, wakijeruhiwa, wakinaswa na kukamatwa.
14
Kwa hiyo sikieni neno la Bwana, enyi watu wenye dharau mnaotawala watu hawa wa Yerusalemu.
15
Ninyi mnajisifu, “Tumefanya agano na mauti, tumefanya mapatano na kuzimu. Wakati pigo lifurikalo litakapopita, haliwezi kutugusa sisi, kwa kuwa tumefanya uongo kuwa kimbilio letu na miungu ya uongo kuwa mahali petu pa kujificha.”

Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.

Settings

Reading style

Typeface

Font size 19px

Reading width 75 chars

Options