Kutoka 18:1-12
1
Basi Yethro, kuhani wa Midiani, baba mkwe wa Mose, akawa amesikia kila kitu Mungu alichomfanyia Mose na watu wake wa Israeli, pia jinsi Bwana alivyowatoa Israeli Misri.
2
Baada ya Mose kumrudisha mkewe Sipora, Yethro baba mkwe wake alimpokea
3
pamoja na wanawe wawili. Jina la mmoja aliitwa Gershomu, kwa kuwa Mose alisema, “Nimekuwa mgeni katika nchi ya kigeni.”
4
Mwingine aliitwa Eliezeri, kwa kuwa alisema, “Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa kutoka upanga wa Farao.”
5
Yethro, baba mkwe wa Mose, pamoja na wana wawili wa Mose na mkewe, wakamjia Mose huko jangwani, mahali alipokuwa amepiga kambi karibu na mlima wa Mungu.
6
Yethro alikuwa ametuma ujumbe kwake Mose, kusema, “Mimi Yethro baba mkwe wako ninakuja kwako pamoja na mke wako na wanao wawili.”
7
Kwa hiyo Mose akatoka kumlaki baba mkwe wake, akainama na kumbusu. Wakasalimiana, kisha wakaingia hemani.
8
Mose akamwambia baba mkwe wake kuhusu kila kitu Bwana alichomfanyia Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na pia kuhusu shida zote walizokutana nazo njiani na jinsi Bwana alivyowaokoa.
9
Yethro akafurahishwa sana kusikia juu ya mambo yote mazuri Bwana aliyowatendea Waisraeli kuwaokoa kutoka mkono wa Wamisri.
10
Yethro akasema, “Sifa na ziwe kwa Bwana, aliyekuokoa wewe kutoka mikononi mwa Wamisri na Farao, na aliyewaokoa watu kutoka mikononi mwa Wamisri.
11
Sasa najua ya kuwa Bwana ni mkuu kuliko miungu mingine yote, kwa kuwa amewatendea hivi wale waliowatenda Israeli kwa ujeuri.”
12
Kisha Yethro, baba mkwe wa Mose, akaleta sadaka ya kuteketezwa na dhabihu nyingine kwa Mungu, naye Aroni pamoja na wazee wote wa Israeli wakaja kula chakula pamoja na baba mkwe wa Mose mbele za Mungu.
Settings