Skip to content
2 Nyakati 28:13-27

2 Nyakati 28:13-27

13
Wakamwambia, “Hamna ruhusa kuwaleta hao wafungwa hapa, ama sivyo tutakuwa na hatia mbele za Bwana. Je, mnataka kuongezea dhambi yetu na hatia yetu? Kwa sababu hatia yetu tayari ni kubwa, nayo hasira kali ya Bwana iko juu ya Israeli.”
14
Hivyo wale askari wakawaacha wale mateka pamoja na nyara mbele ya hao maafisa na kusanyiko lote.
15
Kisha watu waliotajwa kwa majina wakawachukua wale mateka na kutoka zile nyara, wakachukua mavazi wakawavika wale wafungwa wote waliokuwa uchi. Wakawapatia nguo na viatu, chakula na cha kunywa, wakawapa matibabu, wote waliokuwa dhaifu miongoni mwao wakawapandisha juu ya punda, wakawaleta ndugu zao mpaka Yeriko, ndio Mji wa Mitende, kisha wakarudi Samaria.
16
Wakati ule, Mfalme Ahazi akatuma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru kuomba msaada.
17
Waedomu walikuwa wamekuja tena na kuwashambulia Yuda na kuchukua mateka.
18
Pia Wafilisti walikuwa wameshambulia miji iliyokuwa chini ya vilima na katika miji ya Negebu ya Yuda. Nao wakawa wametwaa Beth-Shemeshi, Aiyaloni, Gederothi, Soko pamoja na vijiji vyake, Timna pamoja na vijiji vyake, Gimzo pia pamoja na vijiji vyake na kuishi humo.
19
Bwana aliishusha Yuda kwa sababu ya Ahazi mfalme wa Israeli, kwa kuwa alikuwa ameongeza uovu katika Yuda na kumkosea Bwana mno.
20
Hivyo Tiglath-Pileseri mfalme wa Ashuru akaja kumtesa badala ya kumsaidia.
21
Ahazi akachukua baadhi ya vitu kutoka Hekalu la Bwana, jumba la kifalme na kutoka kwa wakuu wake na kumpa mfalme wa Ashuru kama ushuru, lakini hilo halikumsaidia.
22
Katika wakati wake wa mateso Mfalme Ahazi akazidi kukosa uaminifu kwa Bwana.
23
Akatoa kafara kwa miungu ya Dameski, waliokuwa wamemshinda, kwa kuwa aliwaza, “Kwa kuwa miungu ya mfalme wa Aramu imewasaidia wao, nitaitolea dhabihu ili inisaidie na mimi.” Lakini haya ndiyo yaliyokuwa maangamizi yake na Israeli wote.
24
Ahazi akakusanya pamoja vyombo vya nyumba ya Mungu na kuvivunja vipande vipande. Akafunga milango ya Hekalu la Bwana na kusimamisha madhabahu katika kila njia panda ya barabara za Yerusalemu.
25
Katika kila mji wa Yuda akajenga mahali pa juu pa kuabudia miungu ili kutolea miungu mingine kafara za kuteketezwa na kuchochea hasira ya Bwana, Mungu wa baba zake.
26
Matukio mengine ya utawala wake na njia zake nyingine zote, tangu mwanzo hadi mwisho, zimeandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.
27
Ahazi akalala na baba zake na akazikwa katika Mji wa Yerusalemu, lakini hawakumleta kwenye makaburi ya wafalme wa Israeli. Naye Hezekia mwanawe akawa mfalme baada yake.

Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.

Settings

Reading style

Typeface

Font size 19px

Reading width 75 chars

Options