2 Nyakati 28:1-15
1
Ahazi alikuwa na miaka ishirini alipoanza kutawala. Akatawala huko Yerusalemu kwa miaka kumi na sita. Tofauti na Daudi baba yake, hakufanya yaliyo mema machoni pa Bwana.
2
Akaenenda katika njia za wafalme wa Israeli, na pia akasubu sanamu kwa ajili ya kuabudu Mabaali.
3
Akatoa sadaka za kuteketezwa katika Bonde la Ben-Hinomu, na kuwatoa wanawe kafara kwa kuwateketeza kwa moto, akifuata njia za machukizo za yale mataifa Bwana aliyoyafukuza humo mbele ya Waisraeli.
4
Akatoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia miungu, juu ya vilima, na chini ya kila mti uliotanda.
5
Kwa hiyo Bwana Mungu wake akamtia mikononi mwa mfalme wa Aramu. Waaramu wakamshinda, wakachukua watu wake wengi mateka na kuwaleta mpaka Dameski. Tena alitiwa mikononi mwa mfalme wa Israeli, ambaye aliwaua watu wake wengi.
6
Kwa siku moja Peka mwana wa Remalia aliwaua askari 120,000 katika Yuda, kwa kuwa Yuda walikuwa wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao.
7
Zikri, askari shujaa Mwefraimu, akamuua Maaseya mwana wa mfalme, Azrikamu mkuu wa jumba la kifalme na Elikana aliyekuwa wa pili kwa mfalme.
8
Waisraeli wakawachukua mateka kutoka ndugu zao, watu wapatao 200,000 hawa wakiwa ni wanawake, watoto wa kiume na wa kike. Wakachukua pia kiasi kikubwa cha nyara, ambazo walirudi nazo Samaria.
9
Lakini kulikuwako huko nabii wa Bwana aliyeitwa Odedi, akaondoka ili kukutana na jeshi liliporejea Samaria. Akawaambia, “Kwa kuwa Bwana, Mungu wa baba zenu, aliwakasirikia Yuda, aliwatia mikononi mwenu. Lakini mmewachinja kwa hasira ambayo imefika hadi mbinguni.
10
Nanyi sasa mnakusudia kuwafanya wanaume na wanawake wa Yuda na Yerusalemu watumwa wenu. Lakini ninyi je, hamna pia hatia ya dhambi mliyotenda dhidi ya Bwana Mungu wenu?
11
Basi nisikilizeni! Mkawarudishe mateka mliowachukua kutoka kwa ndugu zenu, kwa kuwa hasira kali ya Bwana iko juu yenu.”
12
Ndipo baadhi ya viongozi katika Efraimu, yaani, Azaria mwana wa Yehohanani, Berekia mwana wa Meshilemothi, Yehizkia mwana wa Shalumu na Amasa mwana wa Hadlai, wakakubaliana na huyo nabii, hivyo wakawapinga wale waliokuwa wanawasili kutoka vitani.
13
Wakamwambia, “Hamna ruhusa kuwaleta hao wafungwa hapa, ama sivyo tutakuwa na hatia mbele za Bwana. Je, mnataka kuongezea dhambi yetu na hatia yetu? Kwa sababu hatia yetu tayari ni kubwa, nayo hasira kali ya Bwana iko juu ya Israeli.”
14
Hivyo wale askari wakawaacha wale mateka pamoja na nyara mbele ya hao maafisa na kusanyiko lote.
15
Kisha watu waliotajwa kwa majina wakawachukua wale mateka na kutoka zile nyara, wakachukua mavazi wakawavika wale wafungwa wote waliokuwa uchi. Wakawapatia nguo na viatu, chakula na cha kunywa, wakawapa matibabu, wote waliokuwa dhaifu miongoni mwao wakawapandisha juu ya punda, wakawaleta ndugu zao mpaka Yeriko, ndio Mji wa Mitende, kisha wakarudi Samaria.
Settings