1 Samweli 20:1-17
1
Kisha Daudi akakimbia kutoka Nayothi huko Rama akamwendea Yonathani na kumuuliza, “Kwani nimefanya nini? Kosa langu ni nini? Nimemkosea baba yako kwa jinsi gani, hata kwamba anajaribu kuuondoa uhai wangu?”
2
Yonathani akajibu, “La hasha! Hutakufa! Tazama, baba yangu hafanyi kitu chochote, kikubwa au kidogo, bila kuniambia mimi. Kwa nini anifiche hili? Sivyo ilivyo!”
3
Lakini Daudi akaapa na kusema, “Baba yako anajua kabisa kwamba nimepata kibali mbele yako, naye amesema moyoni mwake, ‘Yonathani sharti asilijue hili, la sivyo atahuzunika.’ Lakini kweli kama Bwana aishivyo na kama uishivyo, kuna hatua moja tu kati yangu na mauti.”
4
Yonathani akamwambia Daudi, “Chochote unachotaka nifanye, nitakufanyia.”
5
Basi Daudi akamwambia, “Angalia, kesho ni sikukuu ya Mwezi Mwandamo, nami inanipasa kula chakula pamoja na mfalme; lakini niache niende kujificha shambani mpaka kesho kutwa.
6
Kama baba yako akiona ya kuwa sipo, mwambie, ‘Daudi aliniomba sana ruhusa kuwahi Bethlehemu, mji wake wa nyumbani, kwa sababu dhabihu ya mwaka inafanywa huko kwa ajili ya ukoo wake wote.’
7
Kama akisema, ‘Ni vyema sana,’ basi mtumishi wako yu salama. Lakini kama akikasirika, unaweza kuwa na hakika kwamba anakusudia kunidhuru.
8
Lakini kwa habari yako wewe, mtende wema mtumishi wako, kwa sababu mmeingia kwenye agano pamoja naye mbele za Bwana. Kama nina hatia, basi niue wewe mwenyewe! Kwa nini unikabidhi kwa baba yako?”
9
Yonathani akasema, “La hasha! Kama ningekuwa na kidokezo kidogo kwamba baba yangu amekusudia kukudhuru wewe, je, nisingekuambia?”
10
Daudi akamuuliza, “Je, nani atakayeniambia kama baba yako atakujibu kwa ukali?”
11
Yonathani akamwambia, “Njoo, twende shambani.” Basi wakaenda huko pamoja.
12
Kisha Yonathani akamwambia Daudi, “Ninakuahidi kwa jina la Bwana, Mungu wa Israeli, hakika nitamchunguza baba yangu wakati kama huu kesho kutwa! Kama ameweka utaratibu wa kufaa kukuhusu wewe, je, sitakutumia ujumbe na kukufahamisha?
13
Lakini ikiwa baba yangu amenuia kukudhuru, Bwana na anishughulikie kwa ukali, iwapo sitakufahamisha na kukuaga uende salama. Bwana na awe pamoja nawe kama alivyokuwa pamoja na baba yangu.
14
Lakini nitendee wema usiokoma kama ule wa Bwana siku zote za maisha yangu, ili nisije nikauawa,
15
wala usiuondoe wema wako kwa jamaa yangu, hata kama ni wakati ule Bwana atakapokuwa amekatilia mbali kila adui wa Daudi kutoka kwenye uso wa dunia.”
16
Basi Yonathani akafanya agano na nyumba ya Daudi, akisema: “Bwana na awaangamize adui za Daudi.”
17
Naye Yonathani akamtaka Daudi athibitishe tena kiapo chake cha kumpenda, kwa sababu Yonathani alimpenda Daudi kama nafsi yake mwenyewe.
Settings