1 Samweli 20:12-23
12
Kisha Yonathani akamwambia Daudi, “Ninakuahidi kwa jina la Bwana, Mungu wa Israeli, hakika nitamchunguza baba yangu wakati kama huu kesho kutwa! Kama ameweka utaratibu wa kufaa kukuhusu wewe, je, sitakutumia ujumbe na kukufahamisha?
13
Lakini ikiwa baba yangu amenuia kukudhuru, Bwana na anishughulikie kwa ukali, iwapo sitakufahamisha na kukuaga uende salama. Bwana na awe pamoja nawe kama alivyokuwa pamoja na baba yangu.
14
Lakini nitendee wema usiokoma kama ule wa Bwana siku zote za maisha yangu, ili nisije nikauawa,
15
wala usiuondoe wema wako kwa jamaa yangu, hata kama ni wakati ule Bwana atakapokuwa amekatilia mbali kila adui wa Daudi kutoka kwenye uso wa dunia.”
16
Basi Yonathani akafanya agano na nyumba ya Daudi, akisema: “Bwana na awaangamize adui za Daudi.”
17
Naye Yonathani akamtaka Daudi athibitishe tena kiapo chake cha kumpenda, kwa sababu Yonathani alimpenda Daudi kama nafsi yake mwenyewe.
18
Kisha Yonathani akamwambia Daudi, “Kesho ni sikukuu ya Mwezi Mwandamo. Itajulikana kwamba haupo kwa kuwa kiti chako kitakuwa hakina mtu.
19
Kesho kutwa, inapokaribia jioni, nenda mahali pale ulipojificha wakati tatizo hili lilipoanza na usubiri karibu na jiwe la Ezeli.
20
Nitapiga mishale mitatu kando yake, kama kwamba nilikwenda kulenga shabaha.
21
Kisha nitamtuma mvulana na kumwambia, ‘Nenda ukaitafute mishale.’ Kama nikimwambia, ‘Tazama mishale iko upande huu wako! Uilete hapa,’ basi uje, kwa sababu hakika kama Bwana aishivyo, wewe ni salama, hakuna hatari.
22
Lakini kama nikimwambia huyo mvulana, ‘Angalia, mishale iko mbele yako,’ basi inakupasa uondoke, kwa sababu Bwana amekuruhusu uende zako.
23
Kuhusu yale tuliyozungumza wewe na mimi: kumbuka, Bwana ndiye shahidi kati yako wewe na mimi milele.”
Settings